2015-07-03 08:34:00

C.PP.S. Miaka 200 si haba! Wekezeni zaidi kwenye miito ya kimissionari!


Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye pia ni Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa alikuwa ni kati ya Maaskofu waliohudhuria kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya miaka 200 tangu Mtakatifu Gaspar del Bufalo alipoanzisha Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, hapo tarehe 15 Agosti 1815.

Ibada hii imeadhimishwa hapo tarehe Mosi Julai 2015 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, lililoko Jimbo kuu la Roma na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa Familia ya Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu mkuu Rugambwa anasema, hiki ni kipindi cha kumshukuru Mungu kwa wema na uukarimu wake wote aliowajalia Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu katika kipindi cha miaka 200 ya uwepo wao katika maisha na utume wa Kanisa. Anawapongeza kwa kazi kubwa ya kimissionari wanayoitekeleza sehemu mbali mbali za dunia, lakini hususan Barani Afrika wanakofanya utume wao miongoni mwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Itakumbukwa kwamba, Wamissionari wa damu Azizi ya Yesu, Barani Afrika wako nchini Tanzania na Guinea Bissau. Askofu mkuu Rugambwa anachukua nafasi hii kuwapongeza kwa hatua kubwa ambayo wanaendelea kuonesha hususa katika kujitegemea na kuanza kujiongoza wenyewe kama Kanda ya Tanzania, inayotarajiwa kuzinduliwa rasmi hapo tarehe 8 Agosti 2015, katika Makao makuu ya Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania, yaliyoko Jimbo kuu la Dodoma, Tanzania.

Askofu mkuu Rugambwa anakaza kusema, changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, wanahamasisha miito ya kimissionari, ili kuwapata Missionari wengi na watakatifu, watakaojitosa kimasomaso katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha. Kwa njia hii wataweza kuimarisha na kuendeleza maisha na utume wa shughuli za kimissionari ndani na nje ya Bara la Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.