2015-07-02 15:01:00

Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu wafunika Roma! Yaani we acha tu!


Waamini waliokuwa na nyuso za furaha na matumaini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, tarehe Mosi, Julai 2015, majira ya jioni, walikusanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Jimbo kuu la Roma, ili kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa matendo makuu aliyomwezesha Mtakatifu Gaspar del Bufalo kuanzisha Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, miaka mia mbili iliyopita. Shirika hili lilianzishwa hapo tarehe 15 Agosti 1815, nchini Italia, leo hii limeenea sehemu mbali mbali za dunia.

Ibada ya Misa Takatifu ilianza kwa maandamano makubwa na Wakleri waliokuwa wanaongozwa na Askofu mstaafu Joseph L. Charron, C.PP.S. wa Jimbo Katoliki Moines, nchini Marekani, Askofu Erwin Krautler, C.PP.S wa Jimbo Katoliki Altamira-Xingu, Brazil, pamoja na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa. Wakleri walitoka nje, kupokea Masalia ya Mtakatifu Gaspar na kuingizwa Kanisani kwa shangwe na vigelegele vingi kutoka kwa mahujaji wa kitanzania waliolipamba Kanisa kwa vitenge vya picha ya Mtakatifu Gaspar del Bufalo.

Katika utangulizi, Askofu Joseph Charron, alisema, Familia ya Mtakatifu Gaspar ilikuwa imekusanyika kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu kutimiza miaka mia mbili tangu lilipoanzishwa. Haya ni matunda ya ushirikiano wa kimissionari kati ya Mtakatifu Gaspar na Mtakatifu Maria del Mathias, mwanzilishi wa Shirika la Masista Waabuduo Damu Azizi ya Yesu.

Jubilei ya miaka mia mbili ni fursa ya kukumbuka yaliyopita kwa moyo wa shukrani na kuambata ya sasa na yale yajayo kwa moyo wa shukrani unaojikita katika mchakato wa kutaka kuyapyaisha yote kwa kujitahidi kusoma alama za nyakati. Hii ni changamoto kwa Familia ya Mtakatifu Gaspar kujikita katika wito, maisha na utume wao, wakijitahidi kufuata nyayo za Mtakatifu Gaspar, mtume hodari wa Damu Azizi ya Yesu. Changamoto kubwa kwa sasa ni kuambata utakatifu na kuendelea kuwa kweli ni wajumbe na vyombo vya upatanisho, haki na amani. Hii ndiyo tasaufi inayofumbatwa katika Damu Azizi ya Yesu, mto wa rehema.

Askofu Erwin Krautler, katika mahubiri yake alichambua kwa kina na mapana maana ya neon damu katika mazingira ya watu wa nyakati hizi. Damu inaonesha kinzani, vita, nyanyaso na madhulumu; damu ni kielelezo cha utamaduni wa kifo, maafa na majanga mbali mbali yanayoendelea kumwandama mwanadamu. Lakini, damu inapata mwelekeo na maana ya pekee kutoka kwa Yesu Kristo. Damu Azizi ya Yesu ni chemchemi ya maisha  mapya yanayoambata ukombozi ulioletwa na Kristo Yesu.

Damu Azizi ya Kristo ni chemchemi ya upendo wa Baba wa mbinguni, changamoto na mwaliko wa kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai. Damu ya Kristo inaponya na kusafisha roho za watu, tayari kuambata utakatifu unaoshuhudiwa katika maisha. Damu ya Kristo iliyomwagika pale Juu Msalabani ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu. Kutokana na mwelekeo huu mpya, ndiyo maana Mtakatifu Gaspar alitamani kuwa na ndimi nyingi ili kuweze kueneza Ibada kwa Damu Azizi ya Yesu kwa watu wa mataifa, kwani ni Mto wa rehema na mapendo.

Askofu Krautler anakaza kusema, tarehe 15 Agosti 1815 Gaspar akaanzisha Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Giano di Umbria, eneo ambalo lina ushuhuda wa watakatifu wengi ndani ya Kanisa. Hapa Gaspar akajikusanyia Mapadre, akaanzisha Shirika la kazi za kitume linaloambata maisha ya kijumuiya, tayari kuwatangazia watu huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Damu Azizi ya Yesu. Wamissionari wa Damu Azizi wameenea sehemu mbali mbali za dunia, wanaendelea kusimama kidete kutangaza Injili ya huruma, upendo na upatanisho kwa kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Askofu Krautler anasema, leo hii kuna umati mkubwa wa Wakristo unaoendelea kuteseka, kudhulumiwa na kuuwawa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hawa ndio mashuhuda na mashahidi wa imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu wanatumwa kuwa ni vyombo na wahudumu wa upatanisho, haki na amani; wanapaswa kuwa ni Wasamaria wema kwa njia ya huduma makini: kiroho na kimwili, kwa kutetea Injili ya Uhai kama alivyofanya Mwenyeheri Askofu mkuu Oscar Romero.

Mtakatifu Gaspar ameacha ushuhuda mkubwa katika maisha, utume na nyaraka mbali mbali alizoandika. Akafariki dunia akiwa na umri wa miaka 51 tu, lakini nyuma yake ameacha urithi mkubwa wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, ambalo linasherehekea Jubilei ya miaka 200 tangu kuanzishwa kwake. Leo hii Gaspar anawataka Watoto wake kusoma alama za nyakati, ili kweli waweze kuwa ni furaha na matumaini ya watu wanaowazunguka; kwa kuguswa na mahangaiko na mateso ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama wanavyokazia Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu wanapaswa kukuza na kudumisha ari na mwamko wa maisha na utume wa kimissionari, ili kuwatangazia maskini Habari Njema ya Wokovu. Wawe tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi; daima wakisikiliza kilio cha damu na kujitahidi kukipatia majibu muafaka. Wawe ni watu wanaofanya tafakari ya kina na kujitajirisha katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, ili kutoka kifua mbele, tayari Kuinjilisha watu na kuganga mahangaiko yao yanayotokana na dhambi, umaskini, magonjwa na dhuluma. Wawe ni vyombo vya matumaini kwa wale waliokata tamaa na kupondeka moyo, daima wakiambata utakatifu wa maisha.

Askofu Krautler anawataka Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, kumwomba, Mtakatifu Gaspar ili aweze kuwasaidia kupyaisha maisha yao na kuchuchumilia utakatifu wa maisha, ushuhuda makini wenye mvuto na mashiko kwa walimwengu wa nyakati hizi.

Kanisa lilisali matoleo saba kwa lugha mbali mbali ili kuombea ujio wa Ufalme wa Mungu, Uinjilishaji, viongozi wa umma, ili kukuza na kudumisha uadilifu, ukweli na unyofu; kwa ajili ya maskini, wagonjwa na wenye taabu; kwa kuombea haki, amani na usawa bila kuwasahau wote waliotangulia mbele ya haki wakiwa na imani na matumaini katika uzima wa milele. Ibada ilipendeza na watanzania, kama kawaida yao, walishuhudia Injili ya Furaha ikibubujika kutoka katika undani wao. Ibada hii pia imehudhuriwa na DR. James Msekela, Balozi wa Tanzania nchini Italia pamoja na ujumbe wake kutoka ubalozini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.