2015-07-02 15:48:00

Papa Francisko aguswa na mateso ya wananchi wa Ugiriki


Katika kipindi hiki cha mateso na mahangaiko makubwa juu ya mgogoro wa kiuchumi unaoendelea kuitikisa serikali ya Ugiriki, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, utu na heshima ya binadamu vipewe kipaumbele cha kwanza. Haya yamebainishwa na Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican anayebainisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anafuatilia kwa wasi wasi mkubwa majadiliano yanayoendelea kati ya Serikali ya Ugiriki na Umoja wa Ulaya.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na wananchi wa Ugiriki ambao kwa sasa wako njia panda juu ya hatima ya nchi yao kuhusiana na masuala ya uchumi na fedha; mambo ambayo yana madhara makubwa kwa mafao, ustawi na maendeleo ya wengi. Baba Mtakatifu anasema yuko pamoja na wananchi wa Ugiriki, lakini zaidi na familia ambazo zinaendelea kuteseka kutokana na athari za myumbo wa uchumi kitaifa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, utu na heshima ya binadamu vinapaswa kuwa ni kiini cha majadiliano yote ya kisiasa na kitaaluma, ili hatimaye, viongozi waweze kufanya maamuzi yenye busara kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana naye kwa njia ya sala, ili kuwaombea wananchi wa Ugiriki wanaokabiliana na changamoto kubwa katika historia ya nchi yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.  








All the contents on this site are copyrighted ©.