2015-07-02 14:46:00

Mchakato wa kutafuta wadhamini wapigwa madongo!


Mara nyingi kabla ya uchaguzi wa viongozi wa nchi, wagombea urais kupitia vyama vya siasa wanaenda sehemu mbalimbali kujinadisha na kupata wadhamini wa kujiunga na kambi yao. Pahali pengine wanapata mashabiki wengi, lakini sehemu nyingine wanagonga mwamba. Injili ya leo inamwonesha Yesu akiwa na wanachama wachache, anaenda kijijini kwake kutafuta wadhamini lakini anagonga mwamba: “Wengi waliposikia wakashangaa,” yaani walichefuliwa nyongo. Wakahoji maswali yaliyo nje ya sera ili kumnyima udhamini. Mwishoni hata “Yesu mwenyewe akabaki anawashangaa....”Hebu tuyaone mazingira yalivyokuwa.

Wiki iliyopita tuliona matokeo mazuri ya imani ya mama yule wa kutoka damu, na ya ile familia ya mzee Yairo jinsi walivyoachwa wakiyafurahia maisha mapya. Leo tutayaona matokeo ya kukosa imani. Kijiji cha Nazareti kilikuwa na wakazi mia mbili tu. Yesu akiwa na miaka thelathini, akakihama kijiji chake cha Nazareti na kwenda kukaa Kafarnaumu walikompokea vizuri. Leo anaenda kwao ili kuinadisha jumuia yake mpya (mitume) kwa wanakijiji wenzake kusudi wajiunge nayo akitegemea “mcheza kwao hutuzwa.”

Kumbe, siku ya sabato akiwa ndani ya Sinagogi, Yesu alipokabidhiwa maiki na kufundisha ikazuka sintofahamu. “Wengi waliposikia wakashangaa.” Kwa kigiriki kushangaa kutokanako na kufurahi kunaitwa “Ethaumazein (ethaumazo) lakini neno la kigiriki lililotumika hapa ni Ekeplessouto (ekpletto) maana yake kushangaa kwa kushtuka kama vile umetonoswa kidonda. Kwa hiyo, “wengi waliposikia wakachefuka nyongo.” Ingawaje hapa hakijaandikwa alichokisema Yesu, lakini kutokana na maswali yaliyohojiwa, msomaji unaweza kubunia ni lugha na matendo gani yaliyomponza Yesu. 

Yaonekana Yesu aliponzwa pale alipoongea juu ya wema na haki ya Mungu isiyo na upendeleo, kama vile alivyowatembelea makafiri (wapagani) ng’ambo kwa Wagerasi, halafu kuwagusa wakoma, kushirikiana na makahaba na watoza ushuru, kuguswa na mwanamke najisi anayetoka damu, kumshika mkono maiti (yule binti Yairo) nk. Sera za mtindo huo hazikukubalika kabisa na wayahudi waliojisikia kuwa taifa teule na takatifu mbele ya Mungu. Mapato yake kukaibuka maswali potovu yanayomfedhehesha na kuwatia watu chuki dhidi ya  Yesu na sera zake.

Swali mojawapo ni: “Huyu ameyapata wapi haya anayoongea?” Swali hilo linaonesha kuwa wao walikuwa tayari na majibu waliyofundishwa na Wafarisayo, kwamba “matendo ya Yesu yanatoka kwa Belzebul (mkuu wa mashetani).” Kwa hiyo, yasikubaliwe. Kumbe maswali ya msingi yangeweza kuwa kama vile: “Je, ujumbe wa Injili ya upendo, amani na haki unatoa mapato ya pekee au la? Je, alichoongea Yesu ni sawa au si sawa? Je, matendo anayoyafanya ni mema na ya huruma au hapana?” Kama mema basi yanatoka kwa Mungu na hivi tuyafuate.

Swali jingine potovu: “Ni hekima gani hii aliyopewa huyu?” Hapa wanahoji utaalamu wa mtu. Yaonekana hekima ya Yesu haitoki kwa marabi na mafarisayo, yaani haitokani na mfumo wao wa fikra. Kumbe swali la msingi lilitakiwa kuwa “Je, jambo alilosema ni la hekima au la.”

Swali jingine potovu linahusu kazi ya mikono ya Yesu: “Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake? Huyu si yule seremala?” Mseremala, alikuwa mtu maskini, anayepita majumbani mwa watu kurekebisha milango na viti vilivyoharibika ili kupata ridhiki ya siku. Wanauliza asili ya matendo yake ili watu wasizipokee sera zake. Hoja hizo zililenga kumfedhehesha Yesu ili mradi kuzihalalisha fikra zao, na hilo gonjwa ndilo lililokuwa linawatafuna wanyamugi wa Nazareti.

Aina hii ya maswali potovu ipo hadi leo kutoka kwa wanaomchukia Kristu na kanisa lake ili mradi kuwatia watu chuki wasiupokee ujumbe wa Injili – Habari Njema – unaohubiriwa na kanisa. Mathalani wenye chuki na wakristu wanaweza kuyaibua makwazo mbalimbali yaliyowahi kutokea katika historia na hata yale yanayotokea sasa, kuhusu mapadre, maaskofu na viongozi wengine wa kanisa; wataibua vituko vya vita vya msalaba, au madhulumu yaliyofanywa na kanisa katika historia. Lakini wanasahau kwamba makwazo hayo huwezi ukayafananisha na ujumbe mzuri wa Injili aliyoleta Kristu. Swali la msingi juu ya ujumbe wa Kristu lingekuwa: “Je ni ujumbe wa upendo, haki na amani? Je, ujumbe huo ni mzuri au la?”

Maswali potovu unayaona pia katika maisha yetu ya kawaida hata katika siasa au uongozi wa nchi. Tunao viongozi wema na wenye haki na huruma kwa wanyonge na maskini. Viongozi wenye sera za haki na upendo na zenye kujali uhuru wa kila mtu. Kadhalika kuna watu wengi wametoa maisha yao kwa ajili ya kutetea uhuru na haki ya taifa ili kuufanya ulimwengu uwe mpya. Tunayo mifano mingi ya watakatifu na wenyeheri na mapato mazuri ya matendo mema ya Kimungu waliyoyafanya hapa duniani. Hata katika bara letu la Afrika tunayo orodha ndefu ya watakatifu tunaoweza kuwaiga, kama vile Mashahidi wa Uganda, Mtakatifu Josephine Bakhita (Sudan), Mtwenyeheri Clementine Anwarite (Kongo), Mwenyeheri Isidore Bakanja (Kongo), Mwenye heri Viktoria Rasoamanarivo (Madagascar), Mwenyeheri Michael Cprian Tansi (Nigeria), bila kuwasahau Wenyeheri watarajiwa kama vile: Mtumishi wa Mungu Bernadeta Mbawala (Tanzania), Mtumishi wa Mungu Maurice Michael Otunga (Kenya) na Mtumishi wa Mungu Mwalimu Julius K. Nyerere (Tanzania) nk. 

Lakini badala ya kuona matendo mema ya Mungu yaliyotendwa na hawa wenzetu, unashangaa kumwona mmoja anahoji maswali potovu yanayovunjisha moyo na kukatisha tamaa ya kufuata sera na maisha yao ya utu mwema. Kwa mfano badala ya kuhoji na kujadiliana endapo falsafa ya “Ujamaa ni imani” yaani kuujali utu wa kila binadamu, na falsafa ile ya Kujitegemea kama ni nzuri au siyo, watu finyu kama wanyamugi wa Nazareti watakukatisha tamaa na kumwita Mwanafalsafa wake “Mchonga.” Wapi na wapi!

Kuhusu Yesu, wakaendelea kumshushua zaidi waliposema: “Huyu si yule mwana wa Mariamu.” Kwa kawaida Myahudi alijulikana kwa jina la Baba. Kumbe, Yesu anaambiwa ni mtoto wa Mariamu (mama) maana yake ni mtoto wa porini. Halafu “na ndugu zake Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu?” Hayo ni majina ya wazawa wa kiyahudi, yaani ya watu waliozama kwenye mila na desturi za mahali. Inaonesha kuwa Mama na ndugu wote hawakuwa na imani na Yesu, ndiyo maana wakati fulani walienda hadi Kafarnaumu kumchukua wakidhani amerukwa akili.

Kwa hiyo,  “Wakajikwaa kwake yaani wakakwazika naye”. Yesu anajibu: “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake. Mapato yake Yesu “hakuweza kufanya mwujiza wowote huko, isipokuwa aliweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache, akawaponya.” Kumbe imani inatoa mapato mazuri (inaleta maisha mapya) bali kutoamini hakuna mapato yoyote.

Hatimaye, hata “Yesu akastaajabu kwa sababu ya kutokuamini kwao.” Hapa limetumika neno la kigiriki “ethaumazo/ethaumazein” na katika Injili neno hili linapatikana mara thelathini hivi, likimaanisha kushangaa kuzuri mbele ya jambo jipya. Yesu analitumia neno hilo kwa nafasi mbili tofauti: Mosi, anashangaa mbele ya imani ya yule Msenturioni na mara ya pili ni leo anapoishangaa jamii isiyo na imani. Sisi tumdhamini Yesu na tumshangaze kwa kuwa na imani juu yake, na kuiishi Habari Njema.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.