2015-07-02 15:21:00

Binadamu apewe kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya kimataifa


Binadamu, utu na heshima yake ni mambo ambayo yanapewa kipaumbele cha pekee katika kampeni iliyozinduliwa hapo tarehe Mosi, Julai 2015 na Baraza la Kipapa la haki na amani kwa kushirikiana na Shirikisho la kimataifa la Mashirika ya maendeleo kimataifa, CIDSE katika mkutano wake wake wa siku mbili, ambao umezinduliwa rasmi mjini Vatican, tarehe 2 Julai na unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 3 Julai 2015.

Wajumbe wanasema, hapa kuna haja ya kufanya mabadiliko makubwa, ili kukabiliana na changamoto zilizobainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume kuhusu utunzaji bora wa mazingira “ Laudato si”, yaani “Sida kwako” juu ya utunzaji bora wa nyumba ya wote”. Athari za mabadiliko ya tabianchi ni matokeo ya sera tenge, ukosefu wa misingi ya usawa kati ya binadamu, umaskini wa hali na kipato; kwani mambo yote haya  yana athari kubwa katika mabadiliko ya tabianchi.

Wajumbe wakati wa uzinduzi wa kampeni hii wanakaza kusema, ikiwa kama umaskini hautawavilia njuga, sera na mikakati ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi zitagonga mwamba! Binadamu, utu na heshima yake, wanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika mchakato wa mageuzi makubwa duniani, ili kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, yanayoendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao.

Akichangia mada wakati wa uzinduzi wa kampeni hii, Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Flaminia Giovanneli. Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la haki na amani, anasema, katika miaka ya hivi karibuni, Jumuiya ya Kimataifa katika mikutano yake ya kimataifa, imeshindwa kufikia makubaliano yanayotaka kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi. Hii ni changamoto kubwa ambayo inaikabili Jumuiya ya Kimataifa, wakati wa mkutano wa kimataifa juu ya tabianchi utakaofanyika mjini Paris, Ufaransa, kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 11 Desemba 2015.

Hapa kuna haja ya kutambua vikwazo vinavyoendelea kusababisha Jumuiya ya Kimataifa kushindwa kufanya mageuzi makubwa yanayokusudiwa kwa ajili ya kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi. Kardinali Turkson anakaza kusema, tatizo kubwa si masuala ya kiuchumi, kisayansi au kiteknolojia, bali ni watu kushindwa kugeuza akili na mioyo yao, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Bernd Nilles, Katibu mkuu wa Shirikisho la kimataifa la Mashirika ya maendeleo kimataifa, CIDSE, anakaza kusema, mkutano unaoendelea hapa mjini Vatican unawahusisha wadau kutoka katika medani mbali mbali za maisha, ili kuchangia katika changamoto zilizobainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, juu ya utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inafikia maamuzi yanayojikita katika usawa, kanuni maadili na tunu msingi za maisha ya kiuchumi, ili kudhibiti uzalishaji wa hewa ya ukaa ambayo ni tishio kubwa kwa ustawi na maendeleo ya wengi. Hapa kuna haja ya kuibua nishati rafiki itakayosaidia kupambana na uchafuzi wa mazingira pamoja na kuonesha mshikamano wa upendo na nchi changa dunia, ili kuweza kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Huu ni wajibu fungamanishi kwa Serikali, Makampuni na watu binafsi. Hapa mchakato huu hauna budi kuhakikisha kwamba, uhusiano kati ya binadamu na mazingira unakuzwa na kuimarishwa, ili kweli kuleta mabadiliko makubwa yanayokusudiwa duniani. Watu wakielimishwa vyema, wanaweza kuchangia hatua kwa hatua katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira.

Bwana Ottmar Edenhofer, kutoka katika jopo la serikali kuhusu mabadiliko ya tabianchi anafafanua kwamna, Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira unatoa changamoto ya kimaadili na kwamba, majibu ya changamoto kuhusu utunzaji bora wa mazingira yanaweza kupatiwa ufumbuzi, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itashirikiana kwa dhati; kwa kujikita katika majadiliano ya kisayansi, kisiasa, kiuchumi na kidini.

Kwa upande wake, Naomi Klein, mwandishi wa habari za mazingira kutoka Canada, mwana mazingira, ambaye anasema, kwa hakika ameshangazwa sana kupata mwaliko wa kushiriki katika mkutano huu na kwamba, changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira ni kwa watu wote pasi na kuangalia dini au imani yao, kwani athari za mabadiliko ya tabianchi hazibagui wala kuchagua.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu unagusa ukweli na undani wa maisha ya mwanadamu na kwamba, mwanadamu anapaswa kuwa ni mtunzaji bora wa mazingira, vinginevyo, athari za mabadiliko ya tabianchi zinaweza kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, kama inavyoendelea kujitokeza kwa sasa. Binadamu hana budi kufanya mabadiliko, vinginevyo, atajuta kuzaliwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.