2015-07-01 12:04:00

Wabudha na Wakristo shikamaneni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jamii!


Wajumbe kutoka Tume ya majadiliano ya kidini ya Baraza la Maaskofu Marekani, Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini pamoja na wajumbe kutoka katika dini ya Wabudha, wamehitimisha mkutano wao, uliokuwa unafanyika huko Castael Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma, kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 27 Juni 2015. Mkutano huu ulikuwa unaongozwa na kauli mbiu “ Mateso, ukombozi na udugu”.

Mkutano huu wa majadiliano ya kidini umewakusanya waamini wa dini ya Kibudha kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kujadiliana na ndugu zao Wakatoliki kutoka nchini Marekani. Katika tamko lao la pamoja, wajumbe wanakiri kwamba, mkutano huu umewasaidia kukuza mahusiano na ushirikiano wa kiekumene na kidini, kwa kushirikiana na tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu.

Lengo kuu la majadiliano haya ya kidugu, kama alivyosema Baba Mtakatifu Francisko ni kujenga jukwaa jipya la ushirikiano kwa kuwaendea maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuwaonjesha huruma na upendo. Wajumbe wamekubaliana kimsingi kwamba, watakaporejea kwenye miji yao, wataangalia jinsi gani wanavyoweza kushirikiana kwa karibu zaidi kwa ajili ya kutoa huduma kwa maskini; kwa kuangalia jinsi ya kuibua mikakati ya utunzaji bora wa mazingira pamoja na majiundo makini kwa vijana.

Wajumbe wameamua kushirikiana katika masuala ya haki na amani, kwa kuendeleza utume kwa wafungwa magerezani, kwa kuwasaidia wakimbizi na wahajiami; kwa kushirikiana katika kupembua kwa kina na mapana masuala ya kijamii katika maeneo husika; kwa kuendeleza mchakato wa elimu makini kwa familia mbali mbali pamoja na kushuhudia kwa pamoja upendo na mshikamano wa kidugu; kwa kushirikishana tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, ili kuendeleza ushirikiano na waamini wa dini mbali mbali katika miji yao.

Tamko hili limetiwa sahihi na viongozi wakuu kutoka Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini, Tume ya Majadiliano ya kidini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani pamoja na viongozi wa Dini ya Wabudha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.