2015-07-01 08:27:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya XIV ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa


Ni siku nyingine tena tunakutana katika meza ya Neno la Mungu, tukitafakari masomo Dominika ya XIV ya mwaka B wa Kanisa. Mama Kanisa ametuwekea Neno linalotuongoza kutambua nguvu ya Mungu inayojidhihirisha katika walio wanyonge, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, hawa ndio amana ya Uinjilishaji unaotekelezwa na Mama Kanisa sehemu mbali mbali za dunia.

 

Katika Somo la kwanza, tunakutana na sura ya Wana wa Israeli walioasi na kumchukiza Mungu. Pamoja na uasi wao, Mungu bado anawatumia ujumbe wa upendo kwa njia ya Nabii Ezekieli. Mungu anapomtuma Nabii anajua kuwa anamtuma kwa watu wenye mioyo migumu na nyuso zisizo na haya, lakini anasema kwa Nabii, endeni hata kama hawatasikia utakachowaambia, cha msingi watatambua kuwa Nabii yu katikati yao, ishara ya uwapo wa Mungu kati yao.

Mpendwa unayenisikiliza, mwaliko kwetu ni kutangaza Injili ya Bwana pasipo kuanza kujiuliza kutatokea nini au watu watanisikiliza au hapana. Neno la Mungu ni kama mbegu ya haradali iliyo ndogo mno lakini huzaa mti wa ajabu. Kumbe ujumbe wa Neno la Mungu una nguvu ndani mwake pasipo kumtegemea anaye utangaza. Tukumbuke kuwa kila mbatizwa anaitwa kuhubiri Injili pasipo mashaka, pasipo kuwa na matarajio ya ajabu kuliko yaliyo mausia ya Bwana.

Katika somo la Pili, kutoka katika barua ya II ya Mtume Paulo kwa Wakorinto sura 12, Paulo anajivunia udhaifu wake ili uweza wa Kristu ukae juu yake. Anaona mwiba uliokatika mwili wake kama alama ya kudhibiti majivuno ambayo angeweza kufanya kwa sababu ya kazi ya kitume aliyokuwa akitenda. Alimwomba Mungu amwondolee mwiba huu lakini Mungu alimwambia neema yake inamtosha maana uweza wake utimilika katika udhaifu. Ni kwa namna hiyo basi kwa Mtume Paulo shida na madharau ni bure isipokuwa kumjua Kristo ndiko kuna nguvu.

Mwaliko kwetu ni kutambua kuwa katika utume wetu kwa ajili ya Injili kuna vikwazo na madhulumu mbalimbali na Mungu haondoi madhulumu hayo bali hutupa nguvu ya kushindana nayo. Mungu hawaondoi wale wanaohubiri habari njema katika magonjwa na shida za familia zao bali huwapa nguvu za kusonga mbele huku wakivumilia taabu hizo. Kumbe kufaulu katika kazi ya kitume hakutegemei nguvu ya mhubiri bali neema ya Mungu iliyo zawadi siku zote.

Mpendwa msikilizaji, hapo mwanzo tulisema uwezo na nguvu za Mungu hujionesha katika wanyonge, na hivi katika Injili ujumbe huu uko wazi pale ambapo Bwana wetu Yesu Kristu yuko maeneo ya nyumbani kwake, yaani Nazareti akitangaza habari njema na wakati huo watu wakimkataa. Kwa nini wanamkataa, wanamkataa kwa sababu ni mwana wa seremala, ambaye hatarajiwi kutenda miujiza yoyote.

Kwa hakika Seremala alikuwa mtu wa kawaida katika jumuiya ile, kumbe, hakutegemewa kuwa angeweza kuzaa mtoto mwenye hekima namna ile! Watu wa eneo lake badala ya kuangalia Neno la Mungu wanatazama nani anatoa Neno hilo, na hivi wanapotea katika mawimbi ya kiburi chao. Watu hawa badala ya kufuata mausia ya Bwana na kuweza kubadirisha maisha yao, wanabaki katika maoni yao yasiyoleta tija katika mpango wa wokovu. Mwishoni, Bwana akiwatazama kwa upole na wema anawaambia Nabii hakosi heshima katika kazi yake isipokuwa nyumbani kwake.

Mpendwa mwanatafakari, hali hii ni hali ya kawaida katika maisha yetu hivi leo, watu wanabaki kutazama umahili na hata wakati fulani kutazama ujuzi wa mtu badala ya kutazama nguvu ya Neno la Mungu. Mara kadhaa watu wameonesha dharau kwa Wamisionari eti kwa sababu hawatoi pepo!

Mpendwa kutoa pepo si kiini cha habari njema bali ni tendo ambalo Mama Kanisa huratibisha katika safari ya wokovu, ndiyo kusema, Injili ni UPENDO, ni kumjua Kristu na maisha ya fadhila, kiasi kwamba miujiza huja polepole katika maisha ya Kanisa kwa ajili ya sifa na utukufu wa Bwana. Tusisahau kuwa mwujiza hasa huja kwa njia ya upendo kwa Mungu na kwa watu na si kwa njia ya kutoa pepo!

Ninakutakieni heri na baraka tele za Mungu na imani thabiti katika Bwana ukiamini kuwa neema ya Mungu yatosha kwa maisha yako na kwa ajili ya kutangaza Habari njema ukielekeza moyo wako katika ufalme wa mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.