2015-07-01 11:34:00

Papa Francisko anataka kutangaza Injili ya Furaha Amerika ya Kusini


Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 12 Julai 2015 anafanya hija ya kitume kimataifa huko Amerika ya Kusini kwa kutembelea nchi tatu yaani: Equador kuanzia tarehe 5 hadi 8 Julai; Bolivia, kuanzia tarehe 8 hadi 10 Julai na Paraguay, kuanzia tarehe 10 hadi tarehe 12 Julai 2015, Lengo la hija hii ya tisa kimataifa ni kuitangazia Familia ya Mungu Amerika ya Kusini, Injili ya Furaha. Hiki ndicho kiini cha mikusanyiko mikuu itakayofanywa na Baba Mtakatifu wakati wa hija yake ya kitume.

Haya yamebainishwa na Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican wakati alipokuiwa anazungumza na waandishi wa habari mjini Vatican kama sehemu ya maandalizi ya hija ya Baba Mtakatifu Francisko huko Amerika ya Kusini. Tayari ratiba ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Cuba, Marekani na Umoja wa Mataifa mwezi Septemba 2015 imetolewa pia.

Baba Mtakatifu anarejea tena Amerika ya Kusini, baada ya kutimia kwa miaka miwili, baada ya kutembelea kwa mara ya kwanza Brazil kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, iliyofanyika mjini Rio de Janeiro. Wakati huu, Baba Mtakatifu anatembelea Nchi za Amerika ya Kusini zenye utamaduni wa Kihispania na hotuba zake 22 anazotarajiwa kuzitoa, atajimwaga kwa lugha ya Kihispania.

Lengo kuu la Baba Mtakatifu Francisko ni kutaka kukazia kwa namna ya pekee umuhimu kwa Familia ya Mungu katika nchi hizi, kujikita katika mchakato wa ujenzi wa upatanisho, haki na amani; demokrasia na maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Haya ni mambo makuu matatu ambayo yana umuhimu wa pekee katika eneo hili ambalo liko pembezoni mwa Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu anataka kuwahamasisha wajisikie kuwa ni sehemu ya utajiri mkubwa wa Jumuiya ya Kimataifa na kwamba, wanawajibu wa kuchangia katika ustawi na maendeleo yao: kiroho na kimwili.

Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Equador, Bolivia na Paraguay katika kauli mbiu zao, wametoa kipaumbele cha kwanza kwa Injili ya Furaha, ambayo ni kiini cha maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu. Hapa Familia ya Mungu Amerika ya Kusini inataka kuonja na kusikia Injili ya Furaha ikitangazwa na kushuhudiwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume Amerika ya Kusini.

Padre Lombardi anakaza kusema, kutokana na mwelekeo huu, inatarajiwa kwamba, kutakuwa na umati mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema utakaoshiriki katika maadhimisho ya Mafumbo Matakatifu ya Kanisa; mikutano ya hadhara na matukio mengine yaliyopangwa kwenye ratiba yenye utajiri mkubwa kwa maisha na utume wa Kanisa huko Amerika ya Kusini. Baba Mtakatifu ameamua kwamba, kwa kiasi kikubwa anataka kuonana na kusalimiana na wananchi huko Amerika ya Kusini, kumbe, atatumia gari la wazi, ili kuonana na kusalimiana na watu wakati wa matukio mbali mbali.

Padre Lombardi anasema kwamba, ratiba ya Baba Mtakatifu Francisko imebana sana. Anatarajiwa kutumia walau masaa 48 kwa kila nchi pamoja na kutembelea walau miji miwili kwa kila nchi. Maskini, wagonjwa na wazee wanapewa kipaumbele cha pekee wakati wa hija za Baba Mtakatifu huko Amerika ya Kusini. Lakini kila nchi ina mwelekeo wake wa pekee: Equador inatoa kipaumbele cha kwanza kwa wazee; Bolivia kwa wafungwa na Paraguay watoto wagonjwa.

Nafasi kubwa pia itatolewa kwa wenyeji wa mataifa haya, ambao wakati mwingine wanasahauliwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, Baba Mtakatifu anasema, hawa wapewe nafasi ya pekee wakati huu, ili waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, kwani hawa pia ni utajiri mkubwa huko Amerika ya Kusini.

Hii ni safari ambayo itamlazimu Baba Mtakatifu kutumia sana usafiri wa ndege. Padre Federico Lombardi anasema, Baba Mtakatifu hana wasi wasi, anajiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu amtumia kama anavyotaka katika mchakato wa kuwatangazia watu Injili ya Furaha! Kama kawaida, Radio Vatican itakuwa nawe bega kwa bega kukujuza yale yatakayokuwa yanajiri wakati wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko huko Amerika ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.