2015-07-01 12:11:00

Makao Makuu ya APHRC yashinda tuzo ya Idadi ya watu duniani


Kituo cha Utafiti kuhusu Afya na idadi ya watu barani Afrika, APHRC kimepewa tuzo ya Umoja wa Mataifa ya Idadi ya Watu ya Mwaka 2015 katika hafla maalum iliyofanyika kwenye Umoja wa Mataifa, hivi karibuni.

Redio Umoja wa Mataifa, imetaarifu kwamba, kituo cha APHRC chenye  makao yake makuu mjini Nairobi Kenya,  kilicho anzishwa mwaka 1995 kwa ajili ya kusaidia uundwaji sheria kupitia utafiti, kimepata tuzo hiyo kutokana na juhudi zake katika kufuatilia karibu miradi 40 na kwa kusaidia mamia ya watafiti kutoka barani Afrika, kukamilisha masomo yao katika uzamivu au PhD na pia kwa kuchangia katika maswala ya maendeleo endelevu.

Katika mahojiano na Redio ya Umoja wa Mataifa,  Alex Ezeh, Mkurugenzi Mtendaji wa APHCR, amesema tafiti zao zimesaidia nchi mbalimbali kubadili sera, akitoa mfano Kenya, ambako kituo kimeweza  kuchangia katika kufanya mabadiliko kwenye sheria ya uzazi , kwa kutazama kazi zilizo fanyika  nchini Kenya,  kuhusu utoaji mimba usio salama, na kufanikisha kubadilisha sera. Kulingana na ripoti yao ya mwaka 2013, kulikuwa na matukio karibu 500,000 va utoaji mimba usio salama yaliyo tokea nchini Kenya.  Ripoti hiyo,  imesaidia sana kwenye utungaji wa sera na miongozo ya maendeleo kuhusu jinsi ya kukabiliana na changamoto hiyo ya utoaji wa mimba na madhara yake. 

Tuzo ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya idadi ya watu, hutolewa  kila mwaka kwa watu au mashirika yanayo changia kwa kiasi kikubwa katika maswala yanayohusiana  idadi ya watu na afya ya uzazi, Redio Umoja wa Mataifa imetaarifu . 

imeripotiwa na TJ Mhella , Redio Vatican 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.