2015-06-30 08:43:00

Tafiti mbali mbali zinazofanywa ziwafikie walengwa kwa ajili ya mafao ya wengi!


Kitengo cha utume wa vijana kwenye taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu Jimbo kuu la Roma, kinachoongozwa na Askofu msaidizi Lorenzo Leuzzi kwa kushirikiana na Serikali ya Italia, hivi karibuni, kimeendesha kongamano la kumi na mbili la Majaalimu kimataifa, kwa kuwashirikisha wajumbe kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Utu, heshima na mafao ya binadamu ni kati ya mambo msingi ambayo yamepewa kipaumbele cha pekee wakati wa kongamano hili ambalo lilifunguliwa hapo tarehe 25 na kuhitimishwa tarehe 27 Juni 2015 kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Laterano, kilichoko mjini Roma.

Majaalimu kutoka vyuo vikuu kimataifa, wamepembua kwa kina na mapana changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Laudato si”, yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Katika waraka huu, Baba Mtatifu Francisko anatoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu, ustawi na maendeleo yake.

Professa Bruno Botta kutoka Chuo kikuu cha “Sapienza” kilichoko mjini Roma anasema, dunia inaweza kubadilika na kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, ikiwa kama watu watajikita katika mshikamano unaoongozwa na kanuni auni, kwa kuonesha ushirikiano kati ya Majaalim wanaoibukia , wanafunzi na wafanya tafiti, ili wote kwa pamoja waweze kushirikishana uzoefu, ujuzi na mang’amuzi yao, tayari kusaidia mchakato wa maboresho katika sekta ya elimu kwa kukazia utu na heshima ya binadamu.

Hapa, Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kushirikiana kwa karibu zaidi badala ya mtindo uliopitwa na wakati wa kila mtu kufanya mambo peke peke, kwani kuna hatari zake. Jamii ijifunze kujenga na kudumisha utandawazi wa mshikamano kwa kutambua kwamba, watu wanategemeana na kukamilishana, hakuna jamii inayoweza kujidai kwamba, inajitosheleza na kujitegemea kwa kila jambo.

Majaalimu kutoka katika taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu, wanahamasishwa kushirikiana na kushirikishana matokeo ya tafiti zinazofanywa ili ziweze kuwaletea watu mafao na ustawi. Hapa mkazo unatolewa kwenye tafiti ambazo zinagusa kwa namna ya pekee kabisa nishati na teknolojia rafiki, ili kulinda na kutunza mazingira ambayo kimsingi ni nyumba ya wote kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, kuhusu utunzaji bora wa mazingira.

Maji ni rasilimali ambayo inapaswa kutunzwa kwani hii inaweza kuwa ni chanzo cha migogoro na kinzani kwa siku za usoni. Maji ni haki msingi ya binadamu kwani inaambata maisha ya mwanadamu, ustawi na maendeleo yake. Usalama na uhakika wa chakula ni mada nyeti inayoendelea kusumbua akili za wengi katika Jumuiya ya Kimataifa kutokana na ukweli kwamba, leo hii kuna mamillioni ya watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha. Hii ni changamoto endelevu inayopaswa kuvaliwa njuga na wasomi, ili kupata ufumbuzi wa kudumu, unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa maisha ya binadamu na wala si faida.

Athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea bado kutikisa watu wengi pamoja na kuwatumbukiza maskini zaidi katika lindi la umaskini, magonjwa na ujinga pamoja na hali ya kukata tamaa. Hawa ni wale wanaoathirika na matetemeko ya ardhi kila wakati; ongezeko la kiwango cha joto, ukame na mafuriko ambayo yamekuwa ni majanga kwa watu wengi duniani.

Majanga asilia na vita ni kati ya vyanzo vikuu vinavyopelekea watu kukimbia nchi zao, ili kutafuta nafuu na ubora wa maisha sehemu nyingine za dunia, matokeo yake ni wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi, ambalo kwa sasa linaonekana kuwa ni kero kubwa Barani Ulaya na wala si tena rasilimali watu inayoweza kutumika katika uzalishaji na ukuaji wa uchumi. Leo hii, Bara la Ulaya liko njia panda kuhusiana na changamoto ya wahamiaji na wakimbizi.

Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira anasema Bwana Luigi Nicolais, Rais wa Baraza la utafiti kitaifa, nchini Italia uko wazi na unatekelezeka. Ikiwa kama kanuni maadili na kijamii zilizobainishwa na Baba Mtakatifu Francisko hazitatekelezwa kwa dhati, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kujikuta ikiwa inaishi katika ulimwengu utakaokuwa una sheheni majanga na maafa kutokana na ubinafsi na utaifa usiokuwa na tija wala mashiko kwa mafao na ustawi wa wengi.

Watu wajifunze kujenga na kudumisha mshikamano wa kidugu kwa kugawana na kushirikisha raslimali vitu, fedha na watu kwa ajili ya mafao ya wengi. Tafiti zinazofanywa kwenye taasisi za elimu na vyuo vikuu, ziwafikie walengwa, kwa ajili ya ustawi wa familia nzima ya binadamu. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, iwe pia ni fursa ya kushikamana kwa dhati, ili kuoneshana huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu.

Askofu msaidizi Lorenzo Leuzzi, anasema kwamba, wanafunzi na wasomi kutoka katika taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu, wanapaswa pia kusaidiwa kutambua na kuthamini dhana ya huruma ya Mungu, ili wanapotekeleza dhamana na majukumu yao, watambue kwamba, upendo wa kiakili unaojikita katika ufahamu wa mambo mengi, unapaswa pia kutumiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Hii ndiyo safari ambayo Majaalimu wanapaswa kuitekeleza wakati wanapowafunda wasomi wa leo na kesho, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Kongamano hili lilipata baraka na ujumbe kutoka kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia, aliyewatia shime kushikamana na kushirikishana uzoefu na mang’amuzi katika maisha na utume wao kama Majaalimu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.