2015-06-28 16:03:00

Papa Francisko, Karibu sana Bolivia, wanakusubiri kwa hamu!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 28 Juni 2015 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican, alitambua uwepo wa Familia ya Mungu kutoka Bolivia inayoishi mjini Roma pamoja na viongozi wake, waliofika kwa maandamano makubwa, kumtakia heri na baraka kwa ajili ya hija yake ya kichungaji Amerika ya Kusini, ambako atapata nafasi ya kutembelea: Equador, Bolivia na Paraguay kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 13 Julai 2015.

Umati huu mkubwa ulikuwa umebeba Picha ya Bikira Maria wa Bolivia, wakiomba msaada wa daima kwa Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume Amerika ya Kusini. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwatakia heri na baraka vijana wote kutoka Hispania wanaojiandaa kupokea Sakramenti ya Kipaimara, anawasihi kuendelea kumkumbuka katika maisha na utume wake kwa njia ya sala na sadaka zao.

Maandamano ya Familia ya Mungu kutoka Bolivia inayoishi hapa mjini Roma, ilianza tukio hili kwa Ibada ya Misa Takatifu, iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Huruma ya Mungu, ambako wamesali kwa nia ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume huko Amerika ya Kusini. Ibada hii imehudhuriwa na viongozi kadhaa kutoka Bolivia na Vatican.

Baadaye mchana, kumefanyika michezo kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican pamoja na viunga vyake, ili kuonesha utajiri mkubwa wa utamaduni na maisha ya kiroho, unaofumbatwa na kuendelezwa na watu kutoka Bolivia sanjari na kumtakia kila la kheri na baraka, Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume Amerika ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.