2015-06-28 07:47:00

Papa alaani vitendo vya kigaidi huko: Ufaransa, Tunisia na Kuwait!


Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa huko Ufaransa, Tunisia na Kuwait na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Katika ujumbe ulioandikwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Baba Mtakatifu anamwomba Askofu mkuu Luigi Ventura, Balozi wa Vatican nchini Ufaransa, kumfikishia salam zake za rambi rambi kwa wote walioguswa na maafa haya nchini Ufaransa.

Baba Mtakatifu anapenda kuungana na ndugu, jamaa na wanafamilia wote kwa ajili ya kuwaombea waliopoteza ndugu zao katika mashambulizi haya ya kigaidi. Kwa wale waliopatwa majeraha, anawaombea ili waweze kuponya haraka na kurejea tena katkika maisha yao ya kila siku. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, hata wakati huu, bado vitendo vya kigaidi vinaendelea kusababisha maafa makubwa. Anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia watu zawadi ya amani na anapenda kuwapatia baraka zake za kitume wananchi wote wa Ufaransa.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe uliotumwa kwa Askofu mkuu Thomas Yeh Sheng-nan, Balozi wa Vatican nchini Tunisia kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Baba Mtakatifu anasema anapenda kuungana na wananchi wote wa Tunisia waliotikiswa na shambulizi la kigaidi lililosababisha watu kadhaa kupoteza maisha. Anawaombea wote hawa ili waweze kupokelewa na kuonja huruma ya Mungu katika maisha yao.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwaombea faraja wakati huu wa majonzi makubwa. Kwa namna ya pekee, analaani vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kusababisha majonzi makubwa kati ya watu. Anamwomba Mwenyezi Mungu, chemchemi ya amani, aweze kuwakirimia waja wake amani. Mwishoni, anapenda kuwapatia baraka zake za kitume, wale wote wanaoomboleza huko Tunisia.

Baba Mtakatifu Francisko, ametuma pia salam za rambi rambi nchini Kuwait, kutokana na shambulizi la kigaidi lililofanywa kwenye Msikiti, mwishoni mwa juma, wakati waamini walipokuwa wanaswali. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala kwa familia na wote waliotikiswa na janga hili. Anawaombea wote faraja na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwaonjesha upendo wake unaoganga na kuponya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.