2015-06-27 09:15:00

Yesu ni mshindi dhidi ya magonjwa na kifo!


Tunaongozwa na vifungu vifuatavyo katika maadhimisho ya Jumapili ya kumi na tatu ya Mwaka B wa Kanisa: Hek. 1: 13-15; 2: 23-24, 2. 2Kor.8:7.9.13-15, 3. Mk.5:21-43. Tunaona matukio mengi yanayotokea haraka haraka na katika sehemu tofauti. Tukio ukingoni mwa ziwa. Yesu amezungukwa na watu na mtu mmoja anakuja na kuanguka miguuni pake – binti yangu anaumwa sana. Njoo umwekee mikono yako apone na kuishi. Mara Yesu anaacha fundisho alilokuwa akifanya na anaenda nyumbani kwake.

Tukio la pili ni barabarani. Mwanamke anayetokwa na damu anamwendea Yesu, anagusa vazi lake na anapona. Tukio la tatu, wakati Yesu akiongea naye, mara mtu anafika toka nyumba ya Yairo na kumwambia binti yako amekufa, kwa nini wamsumbua mwalimu? Yesu anasikia yote na kumwambia, usiogope. Ni hili ndilo tukio muhimu zaidi katika matukio haya ya leo. Kulikuwa na mfadhaiko na vilio.

Halafu, Yesu anaenda kwenye nyumba na kuingia ndani na anakuta watu wanalia na kuwakemea –kwa nini mnalia? Mtoto hajafa bado ila amelala tu. Anawachukua baba na mama na kwenda alipolala mtoto. Yesu anatoa amri, anamshika mtoto mkono na kumwamuru kuinuka. Mtoto anaamka na kuinuka na kutembea na Yesu anatoa amri kutokutangaza jambo hilo.

Tunaposoma katika maandiko matakatifu, tunaona kuwa lengo kuu la Mungu ni kutoa uhai. Hakika baada ya tafakari hii hapa juu, twaona kuwa maisha si tu uzima tunaouona hapa duniani katika mwili bali yahusisha pia uzima wa roho. Sisi tunatakiwa kusherehekea maisha. Tunu ya uzima toka kwa Muumba. Ule ushirika na Mungu. Ni kuishi na Mungu. Mungu anasema nimekuja ili wawe na uzima – Yoh. 10:10. Kuna aina mbili ya maisha – ya kimwili na ya kiroho. Na maisha ya kiroho ndiyo yanayotugharimu zaidi. Maandiko matakatifu yanapoongea kuhusu maisha yamaanisha aina zote mbili – ya kimwili na kiroho. Mungu anatamani uhai, hivyo kifo si hali ya kimungu. Hii inaonekana kwa ujio wa mwanawe.

Somo la kwanza –haliwezi kusema wazi nafasi ya mwana wa Mungu katika kuleta uhai kwa vile hakujua vizuri habari juu ya Mwana wa Mungu. Ila twaona kuwa Mungu hakufanya kifo na pia hafurahii mwisho wa maisha. Mwandishi anatambua kuwa ulimi wa mwongo huua roho.

Kadiri ya mwinjili Marko, nguvu ya Yesu ni zaidi ya kuponya. Huleta uhai. Ni ufufuko. Mungu wetu ni Mungu wa uzima na mwelekeo wa maisha yetu ni kwenda kwenye uzima. Hapo ufalme wa Mungu huanza – kuwa na uhai, uhai wa mwili na roho. Mzaburi husema,umenipa uhai kati ya waliokuwa wanapotea. Ndicho asemacho mtume Paulo katika somo la pili. Mungu wetu ni Mungu wa uzima. Tunaalikwa kumwamini na kuishi huo ufahamu. Mungu alijitoa kwa ajili yetu. Ndicho alichofanya Yesu hapa duniani. Kutangaza ujio na uwepo wa ufalme wa Mungu, kutupatia uzima wa milele wa kimungu.

Katika Injili:tunaona sherehekeo la uhai. Yule ambaye ana uzima wa kweli, anarudisha maisha kwa kile kilichopotea. Ndicho tunachodaiwa leo na Mungu na watu wake. Je mimi/wewe unao uzima wa kimungu ndani yako? Ambao ndiyo uzima wa kweli? Wale ambao wako katika hali ya kifo, wanaweza kukutafuta ili waupate tena uzima wa kimungu? Katika Gal. 2:20 tunasoma – maisha niishiyo si mimi ila Kristo aishi ndani yangu. Tunaalikwa tutoe nafasi katika maisha yetu ili Kristo atawale. Na utawala wake ni uzima.

Tunatafakarishwa na maisha ya ushuhuda ya Mt. Maximilian Maria Kolbe aliyeuawa wakati wa utawala wa kinazi kwa sababu ya kumshuhudia Kristo. Yeye hakuogopa kifo na hakuogopa dhuluma na kuwa tayari kufa na kushuhudia kuwa kwake kuishi ni Kristo. Msimamo wake kwa imani yake kwa Kristo uliwagusa si tu wafungwa wenzake lakini hata viongozi wa utawala dhalimu. Lao hii tunamheshimu kama mtakatifu.

Ushuhuda wa maisha ya kikristo unatolewa na Padre Joseph Healey, mmisionari wa Maryknoll aliyefanya utume sehemu mbalimbali za Tanzania hasa ukanda wa ziwa, katika kitabu chake ‘Hadithi za Kiafrika” juu ya padre mmisionari aliyefanya utume wake sehemu mbalimbali katika ukanda wa ziwa nchini Tanzania. Siku moja, wakati wa utawala wa Uingereza nchini Tanzania, walitembelewa na mgeni, mtumishi wa serikali. Na kati ya watu walijitokeza kwa wingi kumlaki kiongozi huyo mzungu ni watoto.

Baada ya mgeni mzungu kuondoka, padre aliwauliza watoto sababu ya mshangao wao na kujitokeza kwao kwa wingi kiasi hicho kumwona mgeni. Watoto walijibu wakisema tumemwona mzungu. Padre kwa mshangao mkubwa akawaambia mbona mimi ni mzungu na nimekaa kati yenu muda wote huu. Watoto wakajibu kwa sauti kubwa wewe si mgeni, si mzungu, wewe ni baba yetu. Sote twatambua kuwa nafasi ya mzazi, mlezi ni kutoa uzima.

Tumsifu Yesu Kristo. Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.