2015-06-27 15:35:00

Watakatifu wapya wanne kutangazwa hapo tarehe 18 Oktoba 2015


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Masifu ya hadhuhuri, Jumamosi, tarehe 27 Juni 2015 wakati wa mkutano wa Makardinali, ameridhia kwamba, Wenyeheri wanne, waandikwe kwenye Orodha ya majina ya watakatifu wapya, katika Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa hapo tarehe 18 Oktoba 2015. Itakumbukwa kwamba, hiki ni kipindi ambacho Kanisa litakuwa linaadhimisha pia Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, inayoongozwa na kauli mbiu: “Wito na utume wa Familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo.”

Wenyeheri watakaotangazwa kuwa Watakatifu ni: Padre Vincenzo Gross, mwanzilishi wa Shirika la Masista wa Vituo vya michezo. Sr. Maria wa Bikira Maria mkingiwa Dhambi ya asili, Mama mkuu wa Shirika la Watawa wa “Compagnia della Croce.” Bwana Ludovico Martin, Mlei mwamini na Baba wa familia pamoja na mke wake Maria Azelia Guèrin, Mwamini mlei na Mama wa familia. Hawa ni mifano bora ya kuigwa katika kulinda, kudumisha na kutangaza Injili ya Familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.