2015-06-27 15:48:00

"Ninaomba na kutamani Makanisa yote kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu"


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 27 Juni 2015 amekutana na kuzungumza na ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza, wa Kanisa la Kiorthodox uliowasili mjini Vatican, tayari kushiriki katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa ugeni huu amekaza kusema ni kielelezo cha ushirikiano wa dhati kati ya Makanisa haya mawili; udugu wa damu na imani ulioneshwa na Mtakatifu Petro pamoja Andrea, nduguye, walioungana katika utume na kifo dini. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anamshukuru Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwa mapokeo makubwa aliyomwonesha wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Mtume Andrea, iliyofanyika mwezi Novemba 2014.

Hii ilikuwa ni nafasi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa pamoja  na kuonesha upendo wa kidugu unaoendelea kukoleza hija ya upatanisho, itakayowawezesha Wakristo siku moja kushiriki kwa pamoja maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hii ndiyo changamoto kubwa ambayo Baba Mtakatifu anasema, anaendelea kusali, ili kweli Makanisa yaweze kufikia katika hatua hii. Anapenda kuwahimiza waamini wa Makanisa haya mawili kuendelea kushirikiana na kuheshimiana kwa dhati, ili kuvuka vikwazo na hali ya kudhaniana vibaya ambayo imedumu kwa miaka mingi.

Baba Mtakatifu anasema, lengo ni kuangalia ukweli kwa njia ya moyo wa kidugu, ili kukabiliana na changamoto pamoja na shida ambazo bado zinaendelea kujitokeza. Baba Mtakatifu anaendelea kuunga mkono juhudi za majadiliano ya kiekumene zinazotekelezwa na Tume ya pamoja kati ya Kanisa la Kiorthodox na Kanisa Katoliki. Matatizo yaliyopo yatatuliwe kwa njia ya majadiliano ya kitaalimungu, kwa kukazia dhana ya maisha na utume wa Kanisa; kanuni ya Sinodi na huduma itakayotolewa na kiongozi atakayekuwa na dhamana ya kusimamia na kuratibu umoja wa Makanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anawatakia waamini wa Kanisa la Kiorthodox maandalizi mema ya Sinodi ya Pan-Orthodox na anapenda kuwahakikishia uwepo wake kwa njia ya sala, ili Mababa wa Sinodi waweze kufikia malengo yanayokusudiwa. Baba Mtakatifu anawaomba pia waamini wa Kanisa la Kiorthodox kuwasindikiza kwa njia ya sala Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia na kwamba, anasubiri kwa hamu kuona ujumbe wa kutoka Kanisa la Kiorthodox ukilishiriki.

Baba Mtakatifu ametumia nafasi hii kutoa shukurani zake za dhati kutokana na uwakilishi wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wakati wa kuzindua Waraka wake wa kitume kuhusu utunzaji bora wa mazingira, “Laudato, si” “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji bora wa nyumba ya wote”. Askofu mkuu Giovanni alikuwa ni kati ya wawezeshaji wakuu wakati wa uzinduzi huo uliofanyika mjini Vatican. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwaomba wamfikishie salam na matashi mema, Patriaki Bartolomeo wa kwanza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.