2015-06-26 16:51:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 13 ya Mwaka B wa Kanisa


Ninakuleteeni tena ujumbe wa furaha uletwao na Neno la Mungu, ni Dominika ya kumi na tatu ya mwaka B. Mama Kanisa kwa njia ya Neno la Mungu atuambia Mungu ni maisha na mwanadamu ameumbwa kuishi na si kufa, kumbe tuepuke dhambi chocheo la kifo kwa mwanadamu na tushike imani katika Bwana chanzo uhai na maisha ya milele.

Katika somo la kwanza toka kitabu cha Hekima ya Suleimani ujumbe kwetu ni kuwa Mungu hapendezwi na kifo cha walio hai, kwa maana aliviumba vitu vyote vipate kuwako. Anatumbusha kuepuka dhambi zilizo ashilio la kifo. Anatualika kuifuata ile haki ya Mungu ambayo yaishi milele. Ndiyo kusema kukumbuka daima kuwa Mungu alimwuumba Mwanadamu kwa mfano wake mwenyewe, na hivi asipate kuharibika. Mwaliko kwetu kutunza maisha kwa kuepuka dhambi. Tupambane na uovu ambao umefanya ulimwengu ukaingiliwa na kifo kwa husuda ya shetani!

Mtume Paulo anawaandikia Wakorinto akiwakumbusha kutegemezana katika maisha yao, kuepuka ubinafsi ndiyo kifo kama ilivyosisitizwa katika somo la kwanza. Ndiyo kusema yule aliye na kingi awe ni msaada kwa asiyenacho. Kama Kristu alivyokuwa tajiri na kisha akajifanya maskini basi nao wafanye vivyohivyo katika kutoa utajiri wao wa kiimani na kiuchumi kwa ajili ya wengine. Hivi leo jambo ni lilelile kwetu, tupo katika makundi tofauti, wengine ni Waamini walei, wengine ni Maklero, wengine wamejaliwa zaidi mali ya dunia na wengine mali ya imani, kumbe ili kukamilisha kazi ya Kristu vipaji hivi ni lazima viwekwe pamoja kwa manufaa ya jumuiya.

Katika Injili, Bwana pamoja na Mitume wako katika msafara wa kichungaji. Wanaponya wagonjwa na kuwarudishia waliokufa uhai. Mwinjili ametuwekea mifano miwili ya walio na matatizo na lengo la mifano hii ni kutaka kutupatia nini maana ya kuwa na imani thabiti. Mtu wa kwanza ni Yairo ambaye mtoto wake anaumwa na kabla Bwana hajafika nyumbani tayari binti yake alikwishaaga dunia. Mtu wa pili ni mama mgonjwa aliyekuwa akitoka damu kwa miaka 12 sasa! Hawa watu wawili wanatimiziwa shida zao kwa sababu wanayo imani thabiti katika mponyaji ambaye ni Bwana wetu Yesu Kristo. Yairo ni kati ya wakuu wa Sinagogi, ambao walisadikika kuwa na kiburi kwa sababu ya mamlaka yao, lakini huyu anatambua nguvu ya Mungu inayofumbatwa katika huruma anamkimbilia Bwana na kumwangukia akimwomba amhurumi na amponye mwanae. Bwana anakubaliana na ombi lake na anamrudishia maisha huyu mtoto wa Yairo aliyekwishaaga dunia.

Mama anayetokwa na damu miaka 12 anatambua kuwa akimgusa tu Bwana shida yake itaisha! Anafanya hivyo na anapona. Mpendwa oneni imani ilivyo ya ajabu, yaani kugusa tu mavazi ya Bwana, anapata msaada mkubwa, yaani anaponywa. Anarudishwa katika jumuiya ya watu maana kwa ugonjwa ule asingeweza kushiriki ibada mbalimbali katika Jumuiya ya kiyahudi. IMANI YAKO IMEKUPONYA NDIYO MANENO YA FARAJA ANAYOYASEMA BWANA.

Mpendwa, ninakualika daima kuingia ndani ya maisha yako mwenyewe na kuanza kuona namna gani ukakue katika imani ulio msaada na nguvu yako ya daima na milele. Oneni tendo dogo la kugusa vazi la Bwana lilivyo kielelezo cha imani iliyojaa uthabiti. Ndiyo kusema mambo mengi magumu katika jumuiya tukiyatazama kwa utulivu na unyenyekevu uliojaa imani tutaweza kuyatatua katika Yesu Kristu mganga na mkombozi wa ulimwengu.

Tukutane tena kwa furaha siku nyingine tukitangaza matunda ya imani yetu. Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.