2015-06-26 15:48:00

Kanisa kama Jumuiya liguswe na mateso na mahangaiko ya watu!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Ijumaa tarehe 26 Juni 2015 amekazia umuhimu wa Wakristo kuonesha upendo na mshikamano wa kidugu na watu ambao wanatengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali. Kwa njia hii, Kanisa litaweza kujipambanua kuwa kweli ni “Jumuiya” ya wote.

Yesu katika maisha na utume wake, alikuwa ni kiongozi wa kwanza kuchafua mikono yake kwa kuwaonjesha huruma wagonjwa na maskini pamoja na wote waliokuwa wametengwa na jamii. Kanisa kama Jumuiya ya waamini haina budi kuwa karibu na wote pasi na ubaguzi. Huu ndio ujasiri ulioneshwa na mtu aliyekuwa na ukoma, alipomwomba Yesu akamgusa na kumponya.

Muujiza huu anakaza kusema Baba Mtakatifu unafanyika mbele ya wote kwa kutambua kwamba, mgonjwa wa ukoma alikuwa ametengwa na jamii na tayari alikwisha hukumiwa katika maisha yake kutoambatana na wale waliokuwa safi. Ugonjwa wa ukoma, ulikuwa unaogopesha na ulikuwa ni vigumu sana kuponywa, kama ilivyokuwa vigumu kumfufua mfu.  Hapa Yesu anaonesha ukaribu na uwepo wake kwa mgonjwa mwenye ukoma.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, ni vigumu sana kujenga Jumuiya ya watu pasipokuwepo na mchakato wa ukaribu! Yesu anaonesha ukaribu wake, kwa kumgusa, Yesu anajitwika mateso, magonjwa na mahangaiko ya watu wake. Mtakatifu Paulo anasema kwamba, Yesu hakuona kule kuwa sawa na Mungu ni jambo la kung’ang’ania kwa nguvu, bali alijitwalia hali ya ubinadamu, akawa sawa na binadamu katika mambo yote, isipokuwa hakutenda dhambi. Yesu amejitwika dhambi za walimwengu, ili kuweza kuwa karibu zaidi na binadamu.

Baada ya mtu mwenye ukoma kuponywa ugonjwa wake, anamriwa kutekeleza masharti yaliyowekwa na Jamii kama ushuhuda kwao. Baba Mtakatifu anasema, hatoshi kuwa karibu na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, bali pia kuwashirikisha tena katika maisha ya Kijamii na Kikanisa. Yesu katika maisha na utume wake, kamwe hakumtenga mtu awaye yote! Aliwakumbatia wagonjwa, wadhambi na wote waliotengwa na jamii, akawaonjesha upendo na huruma ya Mungu na kwa njia ya ushuhuda huu makini, watu wengi walivutwa kumfuasa Yesu anasema Baba Mtakatifu.

Kuna kundi kubwa la watu lililokuwa linaangalia kwa jicho la husuda ili kumtia Yesu mbaroni, kumshutumu na kumpaka matope kwa kile ambacho angesema na kutenda. Lakini mgonjwa mwenye ukoma alionesha ujasiri, akathubutu kumsogelea Yes una hatimaye, akaonjeshwa upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani. Hiki ndicho kielelezo makini cha ukaribu wa Kikristo, changamoto ya kuchunguza dhamiri, ili kuangalia ikiwa kama kweli kama Wakristo wako karibu na jirani zao! Je, wanaonesha ujasiri wa kuwasaidia wale wenye shida na mahangaiko ya maisha? Haya ni maswali ambayo yanapaswa kujibiwa na kila mwamini kadiri ya maisha na utume wake ndani ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.