2015-06-25 15:29:00

Wayahudi na Wakristo shikamaneni ili kutetea misingi ya haki na amani!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 25 Juni 2015 amekutana na kuzungumza na ujumbe wa Jumuiya ya Kimataifa ya B’nai B’rirh ambao kwa nyakati mbali mbali ilibahatika pia kukutana na kuzungumza na watangulizi wake. Baba Mtakatifu anasema, haya ni matunda ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, waliochapisha Waraka kuhusu majadiliano ya kidini, unaojulikana kama Nostra eatate, nguzo msingi katika majadiliano ya kidini kati ya Wayahudi na Wakatoliki, kwa kutambua na kuheshimu amana ya maisha ya kiroho inayofumbatwa na waamini wa dini hizi mbili.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, miaka hamsini ya majadiliano ya kidini kati ya Wayahudi na Wakatoliki yanaonesha hatua kubwa ambayo imekwishafikiwa, kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Waamini wa dini hizi mbili wanaweza kushirikiana zaidi kwa ajili ya mafao na ustawi wa binadamu wa nyakati hizi. Waamini hawa katika umoja na mshikamano wao, wanaalikwa kwa namna ya peke, kusimama kidete kulinda na kutetea maisha, utu na heshima ya binadamu. Kulinda na kutunza mazingira; kutetea haki na amani pamoja na kushirikiana kwa ajili ya maendeleo ya jamii nzima, ili kuwajengea vijana wa kizazi kipya matumaini.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, kama waamini wanahamasishwa kwa namna ya pekee: kusali na kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya amani. Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna maeneo mengi duniani ambamo watu wanaishi katika mazingira ya vita, kinzani na migogoro, hali ambayo inajionesha kwa namna ya pekee kabisa katika Nchi Takatifu na huko Mashariki ya Kati. Hapa kunahitajika ujasiri wa kutafuta na kusimamia mchakato wa amani unaopaswa kutekelezwa kwa uvumilivu na subira kwa kuwashirikisha wote, lakini zaidi waamini wa dini hizi mbili.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbuka wale wote ambao wamejitaabisha katika ujenzi wa urafiki kati ya Wayahudi na Wakatoliki. Kwa namna ya pekee, Mtakatifu Yohane wa XXIII, aliyethubutu kuokoa maisha ya Wayahudi wengi waliokuwa wanadhulumiwa wakati wa Vita kuu ya Pili ya Dunia. Ni kiongozi aliyekutana na kuzungumza nao na akaonesha nia ya kuwa na Waraka wa kitume utakaokoleza mchakato wa majadiliano ya kidini.

Mtakatifu  Yohane Paulo II bado anakumbukwa na wengi kwa kutembelea Kambi ya mateso ya Auschwitz pamoja na Hekalu kuu la Roma. Kwa kufuata nyayo za watakatifu hawa, Baba Mtakatifu anapenda kuendelea kuhimiza mchakato wa majadiliano kati ya waamini kama vile alivyoonja na kuguswa mwenyewe alipokuwa Buenos Aires, nchini Argentina.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaombea baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika mchakato wa majadiliano, hasa wakati huu, wanapoadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka wa kichungaji kuhusu majadiliano ya kidini unaojulikana kama “Nostra aetate”, ili urafiki kati ya waamini wa dini hizi mbili ukue na kuzaa matunda kwa ajili ya Jumuiya zao na Familia ya binadamu katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.