2015-06-25 15:44:00

Mtawatambua manabii wa uwongo kwa matendo yao!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 25 Juni 2015 amekazia umuhimu wa viongozi wa Kanisa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini na kuzungumza kwa wastani, kwani hivi ndivyo Yesu alivyowashangaza watu kwa mafundisho yake, kwani alikuwa anafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi wao.

Baba Mtakatifu anasema, waamini wanatambua fika kiongozi ambaye anasema na kutenda kadiri ya Mafundisho ya Yesu, anavyojitahidi kuyamwilisha kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake. Yesu anawaangalisha wafuasi wake kujiadhari na manabii wa uwongo; watu wanaozungumza sana, lakini bila kutenda wala kujenga utamaduni wa kusikiliza. Hapa Baba Mtakatifu akazia umuhimu wa kuzungumza, kutenda na kusikiliza kwa makini.

Hii inatokana na ukweli kwamba, Yesu mwenyewe alikwisha waambia wafuasi wake kwamba, si kila mtu asemaye Bwana, Bwana ataweza kuingia katika Ufalme wa Mungu, bali ayafanyaye mapenzi ya Baba yake wa mbinguni. Kumbe, kuna haja ya kusema, kutenda na kusikiliza kwa makini, ili kukamilisha mchakato unaomdhihirisha kiongozi kuwa kweli ni Nabii kadiri ya vigezo vinavyotolewa na Yesu Kristo anayewataka wafuasi wake, kuhakikisha kwamba, wanaweka katika matendo mafundisho anayowapatia.

Yesu anasema kwamba, mtu yeyote anayesikiliza maneno yake na kuyatekeleza, atafananishwa na mtu mwenye akili aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba thabiti. Hapa waamini wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanasikiliza kwa makini maneno ya Yesu na kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha yao, kwa kutambua kwamba, hapa wanajenga nyumba kwenye mwamba thabiti ambao ni Yesu Kristo mwenyewe.

Manabii wa uwongo wanatambulikana kutokana na matendo yao, kwani ni watu wa maneno mengi, lakini wanatindikiwa na matendo pamoja na utamaduni wa kusikiliza kwa makini. Wanaweza hata kutenda miujiza, lakini hawana moyo wazi wa kusikiliza na kulimwlisha Neno la Mungu katika maisha yao. Ni watu ambao wanaogopa ukimya wa Neno la Mungu, kwani wanakosa msingi thabiti wa maisha yao.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, wachungaji waliomezwa na malimwengu wanashindwa kujenga na kuyakita maisha yao juu ya mwamba wa Neno na upendo wa Mungu; matokeo yake ni kuanguka na kupotea. Kuna haja ya kuzungumza, kutenda na kusikiliza kwa makini, ili kuwa kweli ni Manabii na Wakristo makini, kwa kujenga tabia ya unyenyekevu, utambulisho ulioacha chapa na viongozi wengi wa Kanisa ambao leo hii wamekuwa ni mashuhuri na mifano bora ya kuigwa. 

Kati ya watu hawa ni Mama Theresa wa Calcutta, ambaye alikuwa anatenda katika ukimya, lakini ni mwanamke wa shoka aliyetambua umuhimu wa utamaduni wa kusikiliza kwa makini, ili kuwa na imani inayomwilishwa katika upendo kwa njia ya huduma. Yesu anapenda kuwaimarisha wafuasi wake katika hija ya maisha yao, ili waweze kutambua umuhimu wa kuzungumza, kutenda na kusikiliza kwa makini yale mambo msingi yanayobubujika kutoka katika Neno la Mungu, mwamba wa maisha ya mwamini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.