2015-06-24 17:03:00

Wakimbizi na wahamiaji kutoka Afrika wakutana na Papa Francisko


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu jioni, tarehe 22 Juni 2015 alihitimisha hija yake ya kichungaji Jimbo kuu la Torino kwa kushuhudiwa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wametanda barabarani ili kumpungia mkono wakati anaondoka. Akiwa Uaskofuni, Baba Mtakatifu alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wahamiaji pamoja wakimbizi ambao kwa sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na baadhi ya nchi za Ulaya kufunga mipaka dhidi ya wakimbizi.

Baba Mtakatifu amezungumza na kundi la wahamiaji na wakimbizi ishirini kutoka katika nchi kadhaa za Kiafrika, kwa niaba ya wahamiaji na wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kundi hili limemshukuru Baba Mtakatifu kwa kusimama kidete kuwalinda, kuwatetea na kuwasemea wakimbizi na wahamiaji, maneno yake ni sawa na Oksijeni kwa watu wanaoishi katika mazingira hatarishi na hali ya kukata tamaa ya maisha. Ni maneno yenye matumaini, yanayowapatia ujasiri wa kusonga mbele, licha ya shida na magumu wanayokabiliana nayo. Neno la Mungu ni chemchemi ya imani, matumaini, udugu na mapendo katika hija ya maisha ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu Francisko pia alipata nafasi ya kuzungumza kwa muda mfupi na wanajeshi wa Kikosi cha Zimamoto, kilichokuwa mstari wa mbele katika kuzima moto kati ya tarehe 11 na 12 Aprili 1997 kwenye Kikanisa cha Sanda Takatifu. Moto huo ulisababisha uharibifu mkubwa katika miundo mbinu ya Kanisa kuu na majengo mengine yaliyopo jirani.

Wakati huo, Sanda Takatifu haikuwepo kwenye Kikanisa hicho kwani ilikuwa imehamishiwa kwenye Kanisa kuu. Wananchi wa Torino wanasema, kwa hakika Baba Mtakatifu Francisko amefunika sana , wakati wa hija yake ya kichungaji Jimbo kuu la Torino.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.