2015-06-24 16:21:00

Majadiliano ya kiekumene yaangalie changamoto zilizopo, ili kuwa na ushuhuda


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anakaza kusema, majadiliano ya kiekumene hayana budi kusonga mbele, kama sehemu ya mchakato wa changamoto iliyoanzishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, miaka hamsini iliyopita. Tangu wakati huo, kukaundwa Tume mchanganyiko kati ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni na Kanisa Katoliki.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni wakati huu linaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Tume ya pamoja kati ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni na Kanisa Katoliki ilipoundwa. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko umesomwa kwa niaba yake ya Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa umoja wa Wakristo, Jumanne, tarehe 23 Juni 2015 mjini Roma.

Baba Mtakatifu katika ujumbe huu, anapongeza juhudi ambazo zimefanyika katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita kwa kuboresha mahusiano ya kiekumene kati ya Makanisa, kwa lengo la kutaka kujenga umoja unaonekana wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, licha ya kashfa ya utengano ambayo bado inaendelea kuonekana miongoni mwa Wakristo.

Baba Mtakatifu anawaomba wajumbe wa Tume hii, kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao si tu kwa kuchunguza yale yaliyomo ndani mwao, bali wawe ni jukwaa linalofanya upembuzi yakinifu katika uhalisia wa maisha, kwa kujikita katika ukweli na uwazi, ili kuangalia changamoto zote zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Makanisa, ili hatimaye, kuwasindikiza watu wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na sababu mbali mbali.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linawasaidia watu kuona tunu msingi za maisha na kweli za Kiinjili katika jamii na tamaduni zao. Kuna mateso na mahangaiko mengi ambayo yanatokana na mpasuko miongoni mwa Wakristo, kumbe, hapa kuna haja ya kujikita katika kupembua mada nyeti zinazojikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili hatimaye, Wakristo waweze kuonesha ushuhuda wa umoja hata kama bado haujafikia utimilifu wake. Umoja wa wakristo ni chemchemi na alama ya matumaini duniani na chombo cha upatanisho kati ya Watu wa Mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.