2015-06-24 16:34:00

Kumbu kumbu ya miaka 50 ya ushirikiano kati ya WCC na Kanisa Katoliki


Tume ya pamoja inayoundwa na wajumbe kutoka katika Baraza la Makanisa Ulimwenguni na Baraza la Kipapa linalohamasisha umoja wa Wakristo ni matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, yaliyofungua kwa mara ya kwanza katika historia ya majadiliano ya kiekumene njia inayojikita katika: imani, ukweli na uwazi, ili kulisaidia Kanisa kujenga na kudumisha umoja kamili miongoni mwa Wakristo.

Hiki ni chombo cha pamoja kinachotekeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni na Kanisa Katoliki, kwani Kanisa Katoliki ni mjumbe mtazamaji katika Baraza hili. Tume hii imekuwa ni jukwaa la majadiliano ya kitaalimungu ambayo yanaendelea kumwilishwa katika uhalisia wa maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia.

Mchakato wa majadiliano ya kiekumene unaendelea kujikita katika Uinjilishaji; haki na amani; majiundo ya kiekumene; utume miongoni mwa vijana pamoja na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo. Umuhimu wa tukio hili, umeoneshwa kwa namna ya pekee na Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwengu ambaye, Jumanne, tarehe 23 Juni 2015 ameshiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu Tume ya pamoja kati ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni na Kanisa Katoliki ilipoundwa, kunako mwaka 1965.

Dr. Tveit anakaza kusema, matunda ya kazi zilizofanywa na Tume hii ya pamoja kwa sasa yako mikononi mwa Wakristo, changamoto na mwaliko wa kuendeleza wajibu huu kwa kujikita katika mahusiano mema kati ya Wakristo, ili siku moja, Wakristo wote waweze kuwa mashuhuda wa umoja unaoonekana, kama jibu makini la amri ya Yesu Kristo, ili wote wawe wamoja, ili ulimwengu upate kuamini. Ukweli unabaki kwamba, kuna migawanyiko na mipasuko miongoni mwa Wakristo, kashfa inayoendelea kutawala duniani.

Umoja wa kweli miongoni mwa Wakristo unaweza kuwa ni ujumbe wa imani na matumaini kwa watu wanaoendelea kuteseka kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa; chuki, uhasama na vita bila kusahau athari za mabadiliko ya tabia nchi. Ushuhuda wa pamoja miongoni mwa Wakristo unaweza kuwa ni chombo makini cha ujenzi wa misingi ya haki na amani pamoja na utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote.

Wajumbe wanakaza kusema, majadiliano ya kiekumene katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita yamekuwa na manufaa makubwa kwa Makanisa katika mchakato wa Uinjilishaji na kwamba, Kanisa Katoliki linashiriki kikamilifu kwani kwa sasa Mwenyekiti wa Tume hii ya pamoja ni Askofu mkuu Diarmuid Martin, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dublin, Ireland na kwa upande wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni ni Patriaki wa Kanisa la Kiorthodox kutoka Romania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.