2015-06-23 08:29:00

Papa atembelea Kanisa walimofunga ndoa babu na bibi yake mwaka 1908!


Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa njiani kutoka kwenye Kituo cha Cottolengo kuelekea kwenye Uwanja wa Vittorio ili kuzungumza na bahari ya vijana iliyokuwa imefurika mjini Torino, Jumapili tarehe 21 Juni 2015; Baba Mtakatifu alisimama na kuelekea kwenye Kanisa la Mtakatifu Theresa ambalo liko kati kati ya mji wa Torino, mahali ambapo Babu yake Giovanni alifunga ndoa na Bibi Rosa na baadaye kunako mwaka 1908, Mzee Mario akazaliwa.

Baba Mtakatifu Francisko, ameandika maneno yanayokazia umuhimu wa Injili ya Familia pamoja na Sinodi ya Familia itakayoadhimishwa hapa mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba, 2015.

Kunako mwaka 1929 wazazi wake Baba Mtakatifu Francisko wakahamia nchini Argentina. Mzee Mario Bergoglio alikuwa anafanya kazi kwenye Shirika la Reli nchini Argentina. Akiwa huko akafahamiana na Mama Regina Maria Sivori, wakaoana na kubahatika kupata Mtoto aliyeitwa Jorge Mario, aliyezaliwa tarehe 17 Desemba 1936.

Bibi Rosa Margherita Vassalo Bergoglio ni kati ya watu waliochangia kwa namna ya pekee kabisa malezi ya kiimani, kiutu na kimaadili ya Jorge Mario Bergoglio. Ni mwanamke aliyekuwa na uchaji wa Mungu, akawa kweli ni mwanachama mahiri wa Chama cha Vijana Wakatoliki Italia. Katika shida na mahangaiko yao ya ndani, aliitaka daima familia kukimbilia huruma na upendo wa Yesu kwenye Tabernakulo. Wamwangalie Bikira Maria aliyethubutu kusimama chini ya Msalaba na kupokea maiti ya Mwanaye, Yesu Kristo.

Kwa sala na maombezi ya Bikira Maria, wanaweza kustahimilia shida na mahangaiko yao. Wakumbuke kwamba, “Sanda haina mifuko”. Bibi Rosa alikuwa kweli ni mwanamke wa shoka aliyejitahidi kuwaritisha ndugu zake imani, matumaini na mapendo, leo hii wamekuwa ni kati ya watu wanaoshuhudia imani katika matendo, kama anavyofanya Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.