2015-06-23 09:24:00

Jimbo kuu la Torino: Malengo: Huduma kwa maskini, Umissionari na Neno la Mungu


Wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu Jumapili tarehe 21 Juni 2015 kwenye Uwanja wa Vittorio, Ibada iliyoendeshwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kichungaji ya siku mbili Jimbo kuu la Torino, kuanzia tarehe 21 hadi 22 Juni 2015, Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo kuu la Torino anasema, Familia ya Mungu jimboni humo, imekazia kwa namna ya pekee malengo makuu matatu: Kanisa maskini kwa ajili ya huduma kwa maskini; Mchakato wa maisha ya Kimissionari na Wahudumu wa Neno la Mungu.

Askofu mkuu Cesare Nosiglia, alimwambia haya Baba Mtakatifu Francisko wakati alipohitimisha Ibada ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa na bahari ya watu kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Torino. Haya ni mambo msingi ambayo yamebainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji, Evangelii gaudium, yaani Injili ya Furaha. Umati wa watakatifu na wenyeheri walijipambanua kwa kueneza imani iliyokuwa inajikita katika upendo mkuu unaofumbata Msalaba wa Yesu Kristo.

Ni watu walioshikamana kwa dhati na maskini pamoja na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni watakatifu waliosimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wakaonesha mshikamano wa kidugu unaomwilishwa katika haki, amani na upendo.

Familia ya Mungu Jimbo kuu la Torino, inataka kutoka kifua mbele, ili kushikamana na watu katika makazi yao, wanapochakarika kila siku ili kutafuta mahitaji  yao msingi; mahali wanapoteseka na kutaabika huku wakihangaikia mambo msingi katika maisha; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za kimaadili, kiutu, kiroho na kijamii. Lengo ni kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili.

Askofu mkuu Cesare anasema kwamba, Jimbo kuu la Torino, linataka kuwa kweli ni mhudumu wa Neno la Mungu. Kanisa linataka kuinjilisha kwa njia ya toba na wongofu wa ndani; kwa kuzingatia misingi ya Injili pamoja na kuendelea kuwa waaminifu kwa Injili na imani kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu. Kanisa linataka kuwatangazia watu wa mataifa huruma na upendo wa Mungu, kwa kuonesha ukarimu kwa wale wote wanaojisikia kutengwa na kubaguliwa; hawa ndio wakimbizi, wahamiaji pamoja na wafungwa.

Askofu mkuu Cesare Nosiglia amemkabidhi Baba Mtakatifu sadaka na majitoleo ya waamini na mahujaji waliotembelea na kusali mbele ya Sanda Takatifu, ili sadaka hii isaidie katika mchakato wa Injili ya upendo kati ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.