2015-06-22 16:46:00

Nendeni mkawahudumie vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni, tarehe 21 Juni 2015 aliendelea na hija yake ya kichungaji Jimbo kuu la Torino kwa kukutana na kuzungumza na Wasalesiani na Watawa wa Bikira Maria msaada wa Wakristo, wakati huu, Kanisa linapoadhimisha kilele cha Jubilei ya miaka 200 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Bosco, mtume wa vijana.

Katika hotuba ambayo Baba Mtakatifu Francisko amewakabidhi wanashirika hawa, amekazia kwa namna ya pekee maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Bosco miongoni mwa vijana, hasa zaidi maskini; huduma makini kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, kielelezo makini cha mtawa alijejidhaminisha kwa huruma na upendo wa Mungu katika maisha na utume wake. Imani inapaswa kuwa ni nguzo msingi katika maisha ya watawa, ili kweli huduma ya Injili na kwa ajili ya maskini iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa badala ya kujifungia katika mitazamo yao binafsi katika ulimwengu unaopita kwa haraka na kasi ya ajabu, kiasi cha kuvuka uwepo wao.

Papa Francisko anasema kwamba, maisha ya Mtakatifu Yohane Bosco yalijikita katika huduma kwa vijana, hususan: maskini na wale waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa wakafundishwa imani inayojikita katika kanuni ya maisha ya Wasalesiani yaani, “Kuinjilisha kwa njia ya kuelimisha” na kuelimisha ili Kuinjilisha.

Familia ya Wasalesiani haina budi kuendelea kujikita katika ukarimu na imani; tunu msingi zinazopaswa kuambata mikakati na shughuli mbali mbali za kitume zinazotekelezwa na Wasalesiani sehemu mbali mbali za dunia, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya vijana wa kizazi kipya. Ni mikakati inayomwilishwa katika vituo vya michezo, vituo vya vijana, taasili za kitaaluma, shule, taasisi na vyuo vikuu. Yote haya yafanyike bila kuwasahau vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi. Hawa ni vijana ambao wanahitaji kwa namna ya pekee kuonjeshwa: matumaini na kufundwa katika furaha inayobubujika kutoka katika kisima cha maisha ya Kikristo.

Mtakatifu Yohane Bosco alikuwa ni mnyenyekevu na mwaminifu kwa Kristo na kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Alikuwa tayari kufuata maelekezo aliyopewa na viongozi wa Kanisa katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watoto wa kiroho wa Mtakatifu Yohane Bosco kutoka ili kwenda kukutana na vijana huko waliko kwenye maskani yao; pembezoni mwa miji mikuu; katika maeneo ambamo kuna hatari za maisha ya kiroho na kimwili; katika mazingira ya kijamii ambako kuna uhaba na ukata wa mambo msingi katika maisha. Haya ni maeneo ambayo kimsingi yanakosa: upendo, uelewa, wema na matumaini.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha hotuba yake kwa kuitaka Familia ya Mtakatifu Yohane Bosco, kutoka kifua mbele, ilikuwatangazia Watu wa Mataifa huruma ya Kristo, kwa kutengeneza “vituo vya michezo” kila mahali, lakini kwa wale wanaohitaji zaidi.

Wasalesiani wabebe ndani mwao mtindo wa maisha ya Mtakatifu Yohane Bosco, kwa kuwa na mwelekeo mpana zaidi wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Wamekumbushwa kwamba, leo hii kuna Mashirika mbali mbali ya kitawa yanayoendelea kuishi karama ya Mtakatifu Yohane Bosco, ili kushiriki kikamilifu utume wa kutangaza Injili hadi miisho ya dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.