2015-06-22 16:17:00

Msikubali kuzeeka kabla ya wakati! Changamkieni: upendo, maisha na urafiki


Uwanja wa Vittorio, Jimbo kuu la Torino, Jumapili jioni 21 Juni 2015 ulipambwa kwa nyuso za vijana kutoka sehemu mbali mbali za Italia, waliofika Jimboni hapo ili kusali na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, ili kumshirikisha furaha, matumaini na changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo katika hija ya maisha ya ujana wao. Vijana walifanya maandamano makubwa wakiwa wamebeba Msalaba wa Vijana na Picha inayoonesha watakatifu ambao wamejisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa vijana, kiasi kwamba, leo hii ni chachu ya maisha matakatifu kwa vijana sehemu mbali mbali za dunia.

Katika hotuba ambayo Baba Mtakatifu Francisko aliandaa kwa ajili ya kuzungumza na vijana hao, alikazia mambo makuu matatu: upendo, maisha na marafiki. Haya ni maswali makuu matatu yaliyoulizwa na vijana kutoka Jimbo kuu la Torino na kujibiwa kwa kina na mapana na Baba Mtakatifu Francisko, ambaye kama kawaida, aliweka karatasi pembeni na kuwaanza kuwashirikisha hazina iliyokuwa inabubujika kutoka katika undani wa moyo wake.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kufanya tafakari ya kina kuhusu upendo wa Mungu katika maisha yao; upendo unaowasaidia kuvuka ubinafsi na hali ya mtu kujitafuta mwenyewe na badala yake, upendo unamsukuma mwamini kujitosa kimasomaso kwa ajili ya huduma, ustawi na maendeleo ya jirani zake. Huu ni mchakato unaopania kumsaidia mwamini kuwa ni jirani kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa ni watu wanaoteseka kutokana na upweke katika maisha na kwa njia hii wataweza kugeuza mambo madogo kuwa ni makubwa.

Mtu akijifunga katika ubinafsi wake, atakosa mwelekeo na hatimaye, kukata tamaa ya maisha. Baba Mtakatifu anakaza kusema kwamba, Yesu anawafundisha wafuasi wake kuhakikisha kwamba, wanamwilisha upendo katika uhalisia wa maisha, ili kuweza kuwa na imani na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Mwenyeheri Pier Giorgio Frassati alisikika daima akiwataka vijana kutokubali kuzeeka mapema wangali vijana, bali wajitahidi kuishi bila kuishia!

Kuhusu urafiki na marafiki, Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kuwa kweli ni vyombo vya kutangaza Injili, daima wakitambua kwamba, wao ni matawi na Yesu Kristo ndiye Mzabibu wa kweli, wakiungana na kushikamana naye, wataweza kuzaa matunda ya wema na utakatifu wa maisha; wakijitenga na kumsahau, watakiona cha mtema kuni!

Kwa kushikamana na Yesu, wataweza kupata neema na baraka kutoka kwa Roho Mtaakatifu na hivyo watakuwa kweli: wajasiri, wavumilivu, wanyenyekevu, watu wenye uwezo wa kushirikiana na wengine pamoja na kuwa na ujasiri wa kujitenga na mambo yasiokuwa na mvuto wala mashiko katika ustawi na maendeleo yao: kiroho na kimwili. Kwa kushikamana na Kristo wanaweza kuwapenda hata wale wanaodhani kwamba ni adui za ona hivyo kuwa tayari kujibu ubaya kwa wema. Kwa njia hii anasema Baba Mtakatifu Francisko, vijana wanaweza kuwa kweli ni vyombo vya Uinjilishaji.

Jimbo kuu la Torino, limebahatika kuwa na umati mkubwa wa watakatifu na wenyeheri ndani ya Kanisa. Kwa kuwaangalia watakatifu hawa na kwa namna ya pekee kabisa Bikira Maria, watambue kwamba, mageuzi makubwa ndani ya Kanisa yanapata chimbuko lake katika toba na wongofu wa ndani. Baba Mtakatifu anapenda kuwakumbusha vijana kwamba, upendo mkuu uko kati yao na unaoneshwa kwa namna ya pekee na Yesu Kristo, aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Baba Mtakatifu Francisko akifafanua mambo haya makuu yaani: upendo, maisha na urafiki anawataka vijana kujifunza kutoka kwa Mtakatifu Yohane Bosco, mwalimu, aliyeonesha dhana ya kupenda, akaimwilisha katika huduma kwa kupenda na kuelimisha vijana waliogeuka kuwa ni wenzi wake katika mchakato wa utakatifu wa maisha.

Baba Mtakatifu anasema, vijana wengi wanakosa imani na matumaini kutokana na changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo katika maisha yao yao ya kila siku. Kuna umati mkubwa wa vijana ambao hauna fursa za ajira, kiasi kwamba inakuwa ni vigumu kuweza kupanga na kujiwekea mikakati ya maisha kwa siku za usoni. Jambo la msingi anasema Baba Mtakatifu ni vijana kuchakarika katika maisha, pasi na kukata tamaa wala kwenda pensheni wakiwa na umri wa miaka ishirini.

Vijana watambue kwamba, Mungu ni upendo unaowawezesha kukua na kukomaa katika maisha pamoja na kuhakikisha kwamba, upendo huu unamwilishwa katika uhalisia wa maisha na wala si kubaki kama nadharia, au tai inayoning’inia shingoni! Upendo unajikita katika majadiliano, umoja na kiasi. Upendo unatafuta mafao na ustawi wa jirani, kwa njia ya huduma makini. Msalaba wa Siku ya Vijana Duniani, uwe ni kielelezo cha upendo wa Mungu kwa vijana, tayari kujisadaka kwa ajili ya jirani zao.

Vijana wahakikishe kwamba, wanajenga na kudumisha upendo usiokuwa na unafiki wala maisha ya undumila kuwili; kwa kutangaza amani, lakini wakati huo huo wanawekeza katika uzalishaji na biashara ya silaha ambazo zinaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Huu ndio unafiki ambao umeoneshwa na wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa katika historia ya mwanadamu katika vita kuu ya dunia, mauaji ya kimbari sehemu mbali mbali za dunia pamoja na ukosefu wa uhuru na haki msingi za binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kuwa na imani na matumaini katika maisha, dhidi ya utandawazi na utamaduni usiojali utu na heshima ya binadamu; mambo ambayo yanajionesha kwa namna ya pekee kwa kukumbatia utamaduni wa kifo unaojikita katika sera za utoaji mimba na kifo laini; kwa kutowajali na kuwathamini wazee, kwani hawana tena uwezo wa kuchangia ustawi na maendeleo ya kiuchumi. Matokeo yake ni kushindwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu na binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika mwelekeo huu, vijana wengi wanajikuta wametumbukia katika upweke hasi na utumwa mamboleo; kwa kuwa na matumizi haramu ya dawa za kulevya; kwa kukata tamaa ya maisha na hatimaye, kutema zawadi ya maisha kwa kujinyonga au kwa kuunga mkono vitendo vya kigaidi kama inavyojionesha kwa vijana wengi waliokata tamaa!

Vijana washikamane na kujitahidi kujenga maisha yao pasi na kukata wala kukatishwa tamaa! Wajitahidi kutafuta na kufanya kazi halali, kwa kujikita katika tunu msingi za maisha kiutu, kimaadili na kiroho. Maisha bora hayajengwi kwa matofali ya fedha, raha mustarehe; bali kwa jasho na sadaka. Wawe makini kuchagua mambo msingi katika maisha kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema.

Torino ni kati ya miji ya Italia iliyokuwa na shida na changamoto nyingi za maisha, lakini pia ni mji ambao umezalisha umati mkubwa wa watakatifu na wenyeheri ndani ya Kanisa. Hawa ni watu waliotambua maana ya huduma kwa jirani zao. Baba Mtakatifu anawataka vijana kukita maisha yao katika upendo, maisha na urafiki wa kweli pasi na kukata tamaa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.