2015-06-21 10:49:00

Vita inayoendelea huko Mashariki ya Kati ni uhalifu dhidi ya ubinadamu!


Hivi karibuni, Baraza la Makanisa nchini Canada lilimwandikia barua ya wazi, Bwana Stephen Harper, Waziri mkuu wa Canada, kumtaka aishirikishe Canada katika mikakati ya ulinzi, usalama na msaada wa kibinadamu kwa ajili ya wananchi wa Syria na Iraq ambao kwa sasa wanakabiliana na majanga makubwa ya maisha kutokana na vita inayoendelea huko Mashariki ya kati, vita ambayo kwa sasa imekuwa kama wimbo usiokuwa na kiitikio!

Baraza la Makanisa Canada linasema kwamba, vita inayoendelea huko ni uhalifu dhidi ya ubinadamu na kwamba, waathirika wakuu ni Wakristo ambao wanauwawa pasi na huruma na kulazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na chuki na uhasama wa kidini. Vitendo hivi ni uvunjaji wa haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu na maridhiano kati ya watu.

Baraza la Makanisa Canada linasema kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana kwa dhati na kuweka kando masilahi binafsi, ili kusimama kidete kulinda na kutetea: maisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Viongozi wa Makanisa wanawashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wa Mashirika mbali mbali ya misaada ya kibinadamu wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji huko Mashariki ya Kati, licha ukweli kwamba, wakati mwingine wanahatarisha maisha yao.

Baraza la Makanisa Canada linaiomba Serikali kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidiplomasia pasi na kukata tamaa, ili kukomesha biashara haramu ya silaha huko Mashariki ya Kati, chanzo kikuu cha kinzani na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Hii ni biashara ambayo inanuka damu ya watu wasiokuwa na hatia. Wakimbizi na wahamiaji wanateseka sana, kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kushikamana ili kuwasaidia, kuwalinda na kuwatetea raia dhidi ya mashambulizi ya kigaidi. Kufanyike juhudi za makusudi katika kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ili kuanza mchakato wa haki, amani, maridhiano na upatanisho.

Baraza la Makanisa Canada linabainisha kwamba, mashambulizi ya kijeshi hayawezi kuwa ni suluhu pekee ya vita na kinzani zinazoendelea huko Mashariki ya Kati, kumbe, kuna haja ya kuwa na sera makini kuhusu huduma kwa wahamiaji na wakimbizi pamoja na mikakati ya kiuchumi, bila kusahau kudumisha haki msingi za binadamu, haki na amani.

Waamini wa dini mbali mbali nchini Canada wanaendelea kusali ili kuombea haki, amani na maridhiano na kwamba, majadiliano ya kidini ni jambo ambalo halina budi kuimarishwa ili kujenga na kuimarisha utu na heshima ya binadamu; amani na utulivu. Waamini wengi wana imani katika upendo na huruma ya Mungu; waamini wa dini mbali mbali wajitahidi kufahamiana, kuheshimiana na kusaidiana, ili dunia iweze kuwa kweli ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.