2015-06-21 09:54:00

Papa Francisko: Kazi na Utu wa mtu ni chanda na pete!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuwasili Jimbo kuu la Torino Jumapili tarehe 21 Juni 2015 kwa ajili ya hija ya kichungaji ya siku mbili, kwenye Uwanja wa ndege wa Torino, amepokelewa na viongozi wa Kanisa na Serikali na baadaye akapata nafasi ya kuzungumza na wafanyakazi na wafanyabiashara. Wengi wao ni wale ambao wamepoteza fursa za ajira kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Kuna kundi kubwa la vijana ambao hadi sasa limekata tamaa kutokana na kukosa fursa za ajira. Hawa ndio ambao wamekumbukwa kwa namna ya pekee na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hotuba yake ya kwanza kwa ulimwengu wa wafanyakazi.

Baba Mtakatifu anasema: kazi na utu wa mtu ni mambo msingi sana yanayopaswa kuzingatiwa kwa ajili ya mafao ya wengi. Dhana hii ni muhimu hasa ukizingatia kwamba, Torino ni kati ya miji iliyokuwa na fursa nyingi za ajira, ukawavuta watu wengi kwenda kufanya kazi mjini hapo; hata wahamiaji nao wakapata riziki yao bila shida.

Athari za myumbo wa uchumi kimataifa zinaendelea kuongezeka siku hadi siku, kiasi cha kupungua kwa fursa za ajira na wala wahamiaji hawawezi kulaumiwa kwa kupora fursa za ajira za wenyeji wa mji wa Torino anasema Baba Mtakatifu, kwani wahamiaji nao wanaathirika sana kutokana na ukosefu wa usawa na sera za uchumi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu.

Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu anakemea uchumi usiojali kwani unaendelea kufumbia macho umaskini wa watu ambao kwa sasa umefikia asilimia 10% ya wananchi wote wa Torino. Anawaalika wananchi kutomezwa na malimwengu kwa kutawaliwa na fedha, kiasi cha kuwasukuma watu kutamani utajiri unaofumbatwa katika ubinafsi, matokeo yake ni rushwa na ufisadi pamoja na vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na Mafia.

Wananchi wa Torino wanaoadhimisha kumbu kumbu ya Jubilei ya miaka 200 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Bosco, wamesahau hata mafundisho yake makuu aliyekaza kusema, ukosefu wa usawa kati ya watu ndani ya jamii unasababisha kinzani na mipasuko ya kijamii, kumbe kuna haja kwa wananchi kusimama kidete kuzuia kinzani za kijamii. Kutokana na mateso pamoja na mahangaiko ya wananchi wengi kutokana na ukosefu wa fursa za ajira, Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa kufuata tunu msingi za maisha zilizobainishwa kwenye Katiba ya Italia.

Wananchi wasitegemee "miujiza£ katika mchakato wa kufufua uchumi, bali waanze kushughulikia mikakati itakayowezesha kuwa na mfumo bora wa uchumi unaozingatia mafao ya wengi na wala si kwa ajili ya kupata faida kubwa kwa gharama ya wanyonge ndani ya jamii.

Baba Mtakatifu Francisko anatambua na kuthamini mchango wa wanawake katika shughuli za uzalishaji na uchumi; haki za wanawake katika ulimwengu wa kazi, zinapaswa kuheshimiwa kwani hata katika maeneo ya kazi wanawake bado wanabaguliwa na kutengwa. Hapa wananchi wa Torino wanahamasishwa kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, wanashika usukani katika mchakato wa ukuaji wa uchumi na masuala ya kijamii, kwa kujikita katika mshikamano wa kidugu na majiundo makini ya vijana wa kizazi kipya katika ulimwengu wa kazi.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema kuna haja ya kujenga na kuimarisha mfungamano wa kijamii, kwa kuwajengea tena watu imani; pamoja na kuhakikisha kwamba, wafanyabiashara wanapata mikopo kwa wakati muafaka. Maboresho yanahitajika ili kuonesha uhusiano wa dhati uliopo kati ya elimu na ulimwengu wa kazi. Ni kwa njia hii, watu wanaweza kuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi kiasi hata cha kuchangia kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa ukuaji wa uchumi Torino na maeneo yanayouzunguka mji huu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.