2015-06-21 10:09:00

Jivikeni utu mpya unaoambata wema, upole, huruma, huduma na amani!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuzungumza na ulimwengu wa wafanyakazi mjini Torino, Jumapili tarehe 21 Juni 2015, alikwenda moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Torino, ili kusali na kutoa heshima zake kwenye Sanda Takatifu. Tukio hili limehudhuriwa na Mapadre wazee pamoja na Wamonaki; watu ambao sehemu kubwa ya maisha yao ni sala na tafakari ya Neno la Mungu. Baba Mtakatifu amepata pia nafasi ya kusali kidogo mbele ya kaburi la Mwenyeheri Pier Giorgio Frassati.

Baada ya tukio hili, Baba Mtakatifu alikwenda moja kwa moja kwenye Uwanja wa Vittorio Veneto, ili kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili ya kumi na mbili ya Mwaka B wa Kanisa na kwa namna ya pekee kabisa, katika mahubiri yake amekazia upendo aminifu wa Mungu kwa watu wake; upendo unaoweza kuumba upya, upendo makini na uhaowahakikishia waja wake amani na usalama.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba upendo wa Mungu unajikita katika uaminifu na kamwe hauwezi kudanganya wala kupungua, kwani ni upendo ambao umemwilishwa na kushuhudiwa katika maisha ya Yesu anayeendelea kuwapenda watu wake, kuwavumilia, kuwasamehe na kuwasindikiza katika hija ya maisha. Ni kutokana na upendo kwamba, Yesu, Neno wa Mungu alifanyika mwili, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu na anaendelea kuwa bega kwa bega na wafuasi wake wakati wa raha na shida.

Yesu anapenda pasi na ukomo wala kipimo na kwamba, anaendelea kuwa mwaminifu hata pale wafuasi wake wanapotenda dhambi, anawasubiri kwa hamu, ili kuwasamehe kwani Yesu ni uso wa Baba mwenye huruma. Upendo wa Mwenyezi Mungu unaumba na kuyafanya yote kuwa mapya; kwa kutambua udhaifu na mapungufu ya mtu, tayari kukimbilia msamaha wa Yesu, kwani wokovu unaweza kuingia katika moyo wa mwanadamu, pale tu, anapojiweka wazi mbele ya ukweli, kwa kutambua makosa na dhambi zinazotendwa.

Hapa anasema Baba Mtakatifu kuna haja kwa mwamini kujivua utu wake wa kale unaojikita katika mawazo mabaya na uadui, ili kuwa tayari kujivika utu mpya na safi unaoambata: wema na upole; huruma na huduma kwa jirani pamoja na amani ya ndani. Upendo wa Mungu unadumu na ni salama kwani ni thabiti kama mwamba ambao unaweza kumhakikishia mtu usalama wake pasi na kuanguka. Ni mara ngapi waamini wamejisikia kutokuwa na nguvu ya kusonga mbele, lakini Mwenyezi Mungu daima amekuwa pembeni mwao, akiwa amefumbua mikono na moyo wake ukiwa wazi.

Wananchi wa Torino wanatambua maana ya “mwamba” kwani huu ni ushuhuda ambao unaotolewa na msanii maarufu kutoka Torino Nino Costa katika shairi lake la “Rassa Nostrana” (Razza Nostrana) kwani anafafanua msingi huu na nguvu yake kwa watu wa nyakati zake. Haishangazi anasema Baba Mtakatifu Francisko kuona kwamba, watu wanasahau upendo mkuu wa Mungu na matokeo yake wanajikuta wakielemewa na wasi wasi kwa siku za usoni, kwa kutafuta usalama kwa mambo yanaopita; kujenga jamii inayojifunga ndani mwake badala ya kuwa wazi ili kuwashirikisha wengine.

Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, kwa mfano wa watu waliowashirikisha wengine upendo wa Mungu, kuna uwezekano mkubwa wa kuishi furaha ya Injili kwa kumwilisha huruma; kwa kushirikiana na watu katika shida na mahangaiko yao; kwa kusaidia familia zinazoteseka, lakini kwa namna ya pekee, zile familia ambazo kweli zimeguswa na kutikishwa na myumbo wa uchumi kimataifa. Familia zina hamu ya kutaka kuonja huruma na upendo wa Mama Kanisa, ili ziweze kusonga mbele katika maisha ya ndoa, kwa kutoa malezi na kuwaelimisha watoto wao; kwa kuwatunza na kuwasaidia wazee bila kusahau kurithisha imani kwa vijana wa kizazi kipya.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, kwa msaada wa Roho Mtakatifu, inawezekana kufahamu kwamba, upendo wa Mungu thabiti unawawezesha waamini kuwa imara na wenye nguvu ili kukabiliana na mahangaiko makubwa au madogo katika maisha; upendo wa Mungu unawasaidia kuwa wazi ili kukabiliana kikamilifu na matatizo pamoja na changamoto za maisha kwa ujasiri na kuangalia yajayo kwa moyo wa matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.