2015-06-20 15:51:00

Watu wamegawanyika, wanashindwa kuchangamana na wengine kwa sababu ya chuki!


Wakristo walioko nchini Israeli na Palestina wanaendelea kukabiliana na changamoto nyingi katika maisha yao. Kwanza kabisa kuna shida kubwa ya utashi wa kutaka kuonesha ushuhuda katika ukweli na uwazi; kufahamiana na kuheshimiana; kupokeana na kuendeleza mchakato wa majadiliano; katika mazingira ambamo kuna kinzani, chuki, uhasama na uadui. Haya ni mazingira ambamo watu hawaaminiani, wanaogopana, wanabaguana na kutengana.

Hivi ndivyo Askofu mkuu Giuseppe Lazzarotto alivyopembua na kubainisha, wakati alipokuwa anachangia mjadala katika maadhimisho ya mkutano mkuu wa themanini na nane wa Shirika la Misaada kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, ROACO, ambalo limehitimisha mkutano wake hivi karibuni. Wajumbe walipata nafasi ya kusikiliza upembuzi yakinifu uliotolewa na wahusika mbali mbali kuhusiana na Kanisa huko Mashariki ya Kati.

Wajumbe wameangalia pia hali ilivyo huko Syria, Iraq na changamoto zinazoendelea kujitokeza kwenye Nchi Takatifu. Askofu mkuu Giuseppe Lazzarotto anakaza kusema kwamba, tatizo kubwa linaloendelea kujitokeza kati ya Waisraeli na Wapalestina ni dhana ya uadui, ambayo inatumiwa na wengi, ili kujilinda badala ya kuonana kama ndugu wamoja wanaochangamotishwa kujenga na kudumisha madaraja ya majadiliano ambayo yangewajengea umoja na mshikamano; kwa kutambua mambo mazuri yanayowaunganisha, kuliko kuendelea kung’ang’ania yale mambo yanayowatenganisha na kuwagawa.

Inasikitisha kuona kwamba, wananchi wamegawanyika kiasi kwamba, kila kundi linataka kujihakikishia ulinzi na usalama wake kwa kukataa kuchangamana na wengine. Mwelekeo huu unajenga na kudumisha kuta za utengano wa maisha ya kiroho.

Askofu mkuu Lazzarotto ameelezea mahangaiko ya Wakristo kutoka Iraq waliolazimika kukimbilia nchini Yordan kwa kuhofia usalama wa maisha yao kutokana na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Wanajeshi wa “Isis” ambao wanaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya wakimbizi 7000 na kati yao kuna watoto 1200 ambao wanapaswa kuwa shuleni, lakini hadi wakati huu wanatangatanga na wazazi wao na hivyo inakuwa ni vigumu kuendelea na masomo.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Antonio Franco, anabainisha kwamba, licha ya magumu wanayokabiliana nayo wakristo huko Mashariki ya kati, lakini Chuo kikuu cha Madaba kinaendelea kufanya vizuri katika sekta ya elimu kwani hadi sasa kuna wanafunzi 1600 wanaopata elimu kutoka chuoni hapo.

Naye, Padre Pierbattista Pizzaballa, mhudumu mkuu wa Nchi Takatifu katika taarifa yake, amesema kwamba, kumekuwepo na matumizi makubwa ikilinganishwa na pato lililopatikana. Hii inatokana na maamuzi ya kutekeleza baadhi ya miradi pamoja na kuwasaidia wananchi waliokumbwa na maafa kutokana na mashambulizi yanayoendeshwa na Isis.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.