2015-06-20 16:13:00

Waraka wa Kitume wa Papa Francisko unagusa: Maadili na Masuala ya Kijamii


Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato Si”, yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” uliozinduliwa hivi karibuni, umepokelewa kwa mikono miwili na viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa ni Waraka wenye tunu msingi za maisha ya kiimadili na kijamii. Haya yamesemwa na Rais Sergio Mattarella wa Italia wakati alipokuwa anazungumzia juu ya Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko.

Huu ni mwelekeo chanya kutoka katika uwanja wa wana siasa kuhusiana na utunzaji bora wa mazingira, changamoto endelevu kwa ajili ya kudumisha mafao, ustawi na maendeleo ya wengi. Rais Mattarella anasema kwamba, umefika wakati kwa wanasiasa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya kimataifa, kuliko kunga’ang’ania mafao ya kitaifa peke yake, ili kujenga na kudumisha mshikamano wa umoja, na udugu katika ulinzi na utunzaji wa mazingira, ambayo kimsingi ni nyumba ya wote.

Taarifa kutoka Ikulu ya Italia inaendelea kubainisha kwamba, Waraka huu wa kitume, una mwelekeo unofumbata utandawazi wa mshikamano kati ya watu na kati ya mataifa. Huu ni mwelekeo wa jumla unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika kulinda na kutunza mazingira. Baba Mtakatifu Francisko anaangalia mbali zaidi katika utunzaji bora wa mazingira, ili uweze kuwanufaisha hata watu wa  vizazi vijavyo kwani mazingira ni kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu kuiendeleza kwa ajili yake na kwa ajili ya wengine pia.

Rais Sergio Mattarella wa Italia anahitimisha pongezi zake kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa kuchapisha Waraka wa Kitume kuhusu utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote kwa kusema kwamba, ujumbe huu unawagusa watu wote: wanaoamini na wasioamini, lakini ni ujumbe mahususi kabisa kwa viongozi waliopewa dhamana katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, ili kusimama kidete kwa ajili ya kulinda mafao ya wengi.

Bwana Ban Ki-Moon, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuchapisha Waraka wa Kitume kuhusu utunzaji wa bora wa mazingira kwani hii ni nyumba ya wote. Binadamu wote wana dhamana ya kuhakikisha kwamba, wanalinda na kutunza mazingira kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wote.

Hapa pia kuna haja ya kuonesha mshikamano wa udugu na upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Jumuiya ya Kimataifa ina wajibu wa kuwasaidia watu ambao wameathirika kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabianchi, kwani  waathirika wakubwa mara nyingi ni maskini, ikilinganishwa na watu au nchi zenye uwezo wa kiuchumi.

Rais Barack Obama wa Marekani kwa upande wake, anakiri kwamba,Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote ni ujumbe mzito, unaowawajibisha watu kuhakikisha kwamba, wanalinda na kutunza mazingira kwa ajili ya mafao ya watu wa kizazi cha sasa na kile kijacho, ili kisipate taabu kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ni matumani ya Rais Obama kwamba, Marekani, itakuwa ni kati ya nchi za kwanza kuifanyia kazi changamoto hii kwa ajili ya mafao ya wengi.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa, nchi ambayo itakuwa ni mwenyeji wa mkutano wa kimataifa utakaojadili kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi, utakaofanyika mjini Paris, Desemba, 2015 anasema kwamba, huu ni ujumbe na changamoto ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Jumuiya ya Kimataifa na wala si kwa waamini wa Kanisa Katoliki peke yao. Kumbe, hii ni changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi duniani.

Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato Si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” umepokelewa kwa moyo wa shukrani na viongozi wa kisiasa kutoka katika Nchi za Amerika ya Kusini, ambazo, kimsingi ni kati ya waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi kwa kusema kwamba, viongozi mbali mbali wa kisiasa, wataendelea kuunga mkono juhudi za Baba Mtakatifu katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote. Haya yamesemwa na Rais Juan Manuel Santos Calderòn wa Colombia, ambaye hivi karibuni alikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.