2015-06-20 09:09:00

India yaonesha nia ya kutaka kujenga Reli, ili kupunguza msongamano Dar!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameiomba Serikali ya India kukubali kugharamia ujenzi wa reli katika Jiji laDar es Salaam ili kupunguza misongamano mikubwa ya magari na kuongeza ufanisi wa usafiri katika Jiji hilo.

Ombi hilo la Serikali ya Tanzania limetolewa na Rais Kikwete, Ijumaa, Juni 19, 2015, wakati alipokutana kwa mazungumzo rasmi na Waziri Mkuu wa India, Mheshimiwa Narendra Modi, ikiwa ni sehemu ya shughuli za Rais Kikwete kwenye ziara yake rasmi ya Kiserikali ya siku nne katika India kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Mheshimiwa Pranad Mukherjee.

Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete amemweleza Waziri Mkuu Modi kuhusu jinsi wingi wa magari ulivyoongeza misongamano mikubwa ya magari na hivyo kupunguza sana ufanisi wa usafiri kwa mamilioni ya wakazi wa Jiji hilo. Inakadiriwa kuwa Mji wa Dar Es Salaam una wakazi zaidi ya milioni nne kwa sasa.

Katika maelezo yake, Rais Kikwete ameiomba Serikali ya Modi kufikiria uwezekano wa kugharamia ujenzi wa reli ya juu ya ardhi (siyo ya chini ya ardhi) kama njia ya uhakika zaidi ya kupunguza misongamano. Rais Kikwete amemwambia Waziri Mkuu kuwa tayari amezungumza na Kampuni ya Infrastructure Leasing and Financial Services (IFLS) ya India ambayo imeonyesha hamu ya kushiriki katika ujenzi wa reli hiyo kwa nia ya kuongeza ufanisi wa usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam.

Alhamisi, Juni 18, 2015, miongoni mwa watu wengine, Rais Kikwete alifanya mazungumzo na Mwenyekiti wa ILFS, Bwana Ravi Parthasarathy kuhusu ujenzi wa reli hiyo na Mwenyekiti huyo akaonyesha hamu kubwa ya kufanya hivyo ili mradi Serikali ya India ishauriwe na kukubali kugharamia mradi huo.

Na mwandishi maalum kutoka India.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.