2015-06-19 15:40:00

Wanamichezo dumisheni ushindani wa kweli kwa kujenga mshikamano na udugu


Mama Kanisa anauangalia ulimwengu wa michezo kwa imani na matumaini, kwani anatambua kwamba, hapa ni mahali muafaka pa majiundo makini ya binadamu kwa kujikita katika maisha angavu, mapumziko utu na heshima ya tamaduni pamoja na maisha ya kijamii. Michezo inasaidia ukuaji wa mtu, kwa kutambua uwezo na mapungufu yake kama binadamu. Michezo maalum ya Olympic itakayofanyika mwishoni mwa Mwezi Julai, 2015 inawahusisha watu wenye ulemavu, ili kushiriki katika mchakato unaopania maboresho ya maisha.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na washiriki wa michezo maalum ya Olympic kutoka Italia, Ijumaa, tarehe 19 Juni 2015. Ni jambo la msingi kuona kwamba, watu wenye ulemavu wanashiriki michezo hata katika ngazi ya kimataifa, ili kuweza kuishi kikamilifu maisha yao, jambo ambalo ni changamoto kubwa, ya kuwa na ujasiri wa kusonga mbele licha ya ulemavu ili kugundua nguvu zilizoko ndani mwao na hatimaye, kupenda zawadi ya maisha.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, michezo ni njia muafaka inayowasaidia watu kutoka katika undani wao kwa kushirikiana na wengine, ili waweze kujisikia kuwa kweli ni sehemu hai ya maisha ya kijamii. Kwa njia hii, wanalisaidia hata Kanisa kuondokana na dhana ya ubaguzi na hali ya kuwatenga watu. Huu ni mwaliko kwa wanamichezo kuendelea kuwa waaminifu kwa tunu msingi za michezo na kamwe wasikubali kutumbukizwa katika dhana ya michezo iliyofilisika kwa kujikita katika ufanisi wa kiuchumi, ushindi kwa gharama yoyote ile pamoja na ubinafsi.

Wanamichezo wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanaendeleza dhana ya michezo inayojikita katika tunu msingi za maisha ya binadamu, ushindani katika ukweli wake pamoja na kujenga mshikamano na udugu. Utu na heshima yak ila binadamu, inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza wakati wa michezo, kwa kukuza ukarimu na mikakati ya taasisi mbali mbali pamoja na jamii husika. Baba Mtakatifu anawatakia heri na baraka wanamichezo watakaoshiriki michezo ya kimataifa kuwa na furaha, ari na utulivu, huku wakifurahia pamoja na kujenga urafiki na watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.