2015-06-19 16:21:00

Maaskofu wanamshukuru Papa kwa Waraka wa Kitume kuhusu Mazingira


Kardinali Luis Antonio G. Tagle, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Biblia vya Kanisa Katoliki kwa niaba ya wajumbe waliokuwa wanahudhuria mkutano mkuu wa Shirikissho hili, amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuchapisha Waraka wa Kitume “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Ni matumaini ya Kardinali Tagle kwamba, waraka huu utaweza kuamsha ndani ya Familia ya Mungu ari na mwamko wa utunzaji bora wa mazingira.

Kardinali Tagle anasema, iwe ni nafasi kwa wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuwajibika barabara kwa kuonesha mshikamano wa upendo na udugu kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili wao pia waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Wajumbe wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuonesha ari na moyo wa kimissionari tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, kwa kutambua kwamba, kwa asili Kanisa lina dhamana na wajibu wa Kimissionari wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kwa kujishikamanisha na Kristo Yesu na wala si kwa fedha, dhahabu na almasi. Mihimili ya Uinjilishaji hai na budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Neno la Mungu, ili kuwatangazia Watu wa Mataifa kwamba, Ufalme wa Mungu umewadia na tayari uko kati yao.

Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji mpya. Neno hili linapaswa kusomwa, kutafakariwa na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha, ili kuwaonjesha watu huruma, upendo na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Wajumbe wanamwomba Baba Mtakatifu Francisko kuwasindikiza katika dhamana yao kwa njia ya sala na sadaka yake, ili kweli waweze kuongozwa na Neno la Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.