2015-06-17 16:12:00

Yewooomi! Ye waka! Boss kauchapa usingizi, chombo kinakwenda mrama!


Kuna hoja nyingi zinazosababisha ajali za safari za angani, za barabarani, za majini hata za miguu. Nyingi ya ajali hizo husababishwa na ubovu wa chombo, lakini hasahasa hutokana na miundombinu mibaya, hata machafuko ya hali ya hewa angani na ya bahari. Lakini pia msababishaji mwingine mkubwa wa ajali anaweza kuwa dereva au rubani anapojisahau au anapopitiwa na lepe la usingizi wakati akiendesha. Dereva huyo asiposhtuliwa chombo kinakula mkenge na wasafiri wote mnaangamia.

Dereva, nahodha na rubani wa chombo cha usafiri anaweza kulinganishwa na Muasisi wa nchi, anayelipigania uhuru taifa lake toka kwa wakoloni, na baada ya uhuru anajaribu kuliundia falsafa ya maisha. Muasisi huyo anakuwa kama Musa alivyofanya kwa Taifa la Wayahudi, akalitungia hata amri. Kadhalika muasisi kadiri anavyolifahamu taifa lake, analitengenezea dira kamambe lipate kuwa na utamaduni wake, na hivi kulielekeza kwenye hatima ya maendeleo, ya haki na amani akilitahadharisha pia dhidi ya maadui wa Taifa. Muasisi akifariki fikra na sera zake zinabaki.

Warithi wa uongozi wanatakiwa kuzifuata fikra za mhasisi kwa vitendo na kuziendeleza, yaani “kumwenzi mhasisi.” Kufanya hivyo ni sawa na kuamsha falsafa yake na Muasisi anaonekana bado anaishi ingawa amekufa. Bila kuamsha fikra na falsafa za Muasisi na kuziishi, hapo Taifa linakosa dira na mwelekeo na mapato yake linakula mkenge. Hapo ndipo yanapoibuka maswali, “Huyu dereva au nahodha ni wa namna gani? Muasisi alitaka kulipeleka wapi Taifa? Huyu kiongozi tuliye naye sasa ni wa namna gani?

Maswali kama haya ndiyo yanaulizwa leo na Mitume wa Yesu baada ya kuhangaika muda mrefu na mashua iliyokuwa inakaribia kula mkenge kutokana na dhoruba kali. Walipokuwa wanahaha hivyo, kumbe kiongozi wa msafara na rubani wa meli hiyo alikuwa kwenye shetri au wanaita tesi yaani sehemu ya nyuma ya meli panapokaa usukani unaoongoza meli inakotakiwa kuelekea. Walipoenda kumwangalia wakamkuta rubani mwenyewe amelaza kichwa juu ya mto anautwanga usingizi.

Budi ikumbukwe pia kwamba, kabla ya kutokea patashika hizi, Yesu alikuwa amefanya kazi mchana mzima alipotoa na ile mifano miwili ihusuyo mbegu. Baada ya mfano huo wa  mpandaji kulala akiacha mbegu ichipue yenyewe, sasa Yesu mwenyewe analala wakati chombo chake kinasafiri. Kwa hiyo endapo swali la wakati ule lilihusu hatima ya mbegu au mstakabali wa sera za kampeni yake, leo kuna kujibu swali linalomhusu Yesu akiwa kama mhasisi wa sera hiyo: “Hivi huyu ni nani?”

Ili kujibu ipasavyo swali hilo hatuna budi kuangalia kwa makini maana ya matendo na picha za kibiblia zilizotumika katika fasuli hii kama vile, wakati na mahali pa tukio, chombo (Mashua), mawimbi, upepo, giza la usiku, bahari, kulala usingizi, mto, imani, hofu nk. Picha hizo zinaweza kutupatia mwanya wa kuelewa maana ya fasuli hii ya leo.

Nyakati kilipotokea kimbembe hiki ni za jioni kama inavyosimuliwa: “Kulipokuwa jioni” maana yake, mwisho wa siku, mwisho wa kazi ya Yesu, hasa baada ya kuongea kwa mfano juu ya ufalme wa mbinguni au hata ukitaka kumaanisha mwisho wa maisha haya. Badala ya kwenda kupumzika Yesu na mitume wake wanaanza safari ya kwenda ugenini kwa wapagani, tena safari ya majini.

Kuhusu mahali, Yesu akasema: “Na tuvuke mpaka ng’ambo,” yaani kuvuka ziwa la Tiberia (Galilaya) kutoka Kafarnaumu kijiji kilichokuwa ziwani hapo alipokuwa anakaa nyumbani kwa Petro, hadi kijiji cha Gerase kilicho ng’ambo yake, huko walikaa wapagani. Toka Kafarnaum hadi Geraseno siyo parefu sana kusafiri na yaweza kuchukua muda wa dakika arobaini na tano hivi kuvuka kwa mashua. Yesu aliposema, “na tuvuke ng’ambo,” maana yake kwenda kupeleka Habari Njema (Injili) kwa wakazi wa ng’ambo nyingine waliko wapagani ili nao waweze kuisikia na kuiishi.

Kuhusu Yesu kulala usingizi ndani ya mashua, yasemwa pia kuwa mashua waliyosafiria ilikuwa ndogo ya kuwatosha yeye na mitume wake. “Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakalipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto.” Katika mazingira kama hayo, wakati mitume wanahaha, inashangaza kumwona nahodha analala usingizi. Katika Biblia  usingizi unamaanisha kifo. Kwa mfano, jumapili ijayo, tutasikia Yesu anasema kuwa “binti Yairo hajafa bali amelala.” Kadhalika alipoenda kumhuisha Lazaro alisema kuwa “lazaro amelala hajafa.” Halafu “mto” kwa kawaida huo ulikuwa unawekwa kutegemeza  kichwa cha maiti.

Kuhusu mawimbi na dhoruba, hizo ni alama ya vurugu za maisha, kwani ziwa au bahari husadikiwa kuwa ni makao ya shetani, pepo wabaya, majini na maadui wa kila aina. Kijumla machafuko ya bahari, yaani dhoruba na upepo wa mbisho vyamaanisha wapinzani wa amani na utulivu wa maisha ya binadamu. Dhoruba hizo tunaweza kuzilinganisha pia na vita, ufisadi, uovu wa kila aina, rushwa, ubaguzi wa ukabila, udini, ubaguzi nwa utofauti wa rangi ya ngozi, unyanyasaji wa jinsia, uchakachuaji wa sera au falsafa njema za wahasisi nk.

“Chombo kikajaa maji mengi na kulikuwa na dhoruba kali,” maana yake ni upinzani mkali unaozuia ujumbe wa Injili usipite, hivi sera za mhasisi zisivuke. Ni sawa kama vile bahari ingesema “Hapiti mtu hapa!” Huo ni upinzani dhidi ya nguvu au sera za Yesu zinazojenga ulimwengu mpya, kwani ulimwengu wa kale unataka kuendelea na sera zake za kipagani. Kuhusu mashua, hicho ni chombo kinachomaanisha jumuia kama kilivyokuwa chombo cha Noe. Kwa hiyo Yesu baada ya kutangaza Neno lake (Ufalme wa Mungu) analala ndani ya mashua. Mashua au jumuia hiyo ipo katika kipindi ambapo Yesu yuko lakini amelala  (amekufa).

Katika maisha mara nyingi Mungu anaonekana kama vile hayuko, na mtu anabaki anauliza maswali kama tunavyosali na mzaburi “Ee Bwana hata lini utaniahau, hata milele? Hata lini utanificha uso wako? Hata lini adui yangu atukuke juu yangu?” (Zab. 13:1-2).  “Je, Yesu yuko au amelala?”

Tunapokabiliwa na dhoruba nzito za maisha, tunamtaka Mungu anayetoa amri na kuamrisha kunyamaza dhoruba mbalimbali za maisha. Kumbe, hatutambui kuwa dhoruba hiyo inatokea pale tunapomwacha Mungu au Kristu aliye ndani mwetu alale usingizi. Tunamwacha alale kama mfu juu ya mto wa mioyo yetu, yaani tunafanya mambo yetu kama vile Yesu asingekuwepo. Lakini kumbe kama tunamwamsha, tunasali na kumwomba, yeye anao uwezo wa kutuliza dhoruba tunayoionja katika maisha. Kama hatumwamshi dhoruba itaendelea kutuyumbisha. Mathalani tukimsahau na kumwacha alale wakati tunapokoseana haki, tunapozama kwenye marahamaraha ya maisha, katika kujilimbikizia mali, hapo tunakula mkenge. Kumbe tumwamshe Kristo, tuamshe Neno la Injili yake mioyoni mwetu.

Onyo hili linaelekezwa pia kwa Taifa linaloziua fikra au falsafa ya muasisi wake na kuzizika katika kaburi la sahau, matokeo yake linayumbishwa na dhoruba na mawimbi ya aina nyingi ya sera. Taifa “Linakuwa bendera fuata upepo.” Mapato yake linakula mkenge na kufa katika wimbi la kumwagana damu zitokanazo na utofauti wa rangi za ngozi, ukabila, dini, rushwa,  nk. Taifa likishakula mkenge ndipo linaanza sasa kukumbuka kuziamsha falsafa za mhasisi. Hapo lina kuwa limeshachelewa na “majuto ni mjukuu.”

Ujumbe mwingine tunaopata hapa, ni kwamba tunapomchukua Kristo (Injili) katika Jumuia zetu na kumpeleka au kumhubiri ng’ambo katika nchi ya wapagani, tunaweza kupambana na dhoruba kali na upepo wa mbisho, shetani, majini yaani, wapinzani. Basi hapo tusisahau kwamba Yesu yupo nasi. Yesu peke yake anaweza kuyagombeza mawimbi na dhoruba kama vile anamgombeza shetani. Hapo ndipo tutakapojaa mshangao kama wa mitume na kuhoji: “Ni nani huyu, basi hata upepo na bahari humtii?” Kwa vyovyote huyo ni Mungu peke yake anayeweza kufanya hivyo. Tukitaka kuaminisha maisha yetu kwa Kristo budi tutambue yeye ni nani, ndiye anayeweza kuzima dhoruba zote za maisha.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.