2015-06-17 16:32:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 12 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa


Mpendwa mwana wa Mungu, tunaendelea na tafakari yetu kama kawaida na leo tuko Dominika ya kumi na mbili ya Mwaka B. Neno la Mungu latualika kutafakari juu ya nguvu ya Kristu dhidi ya mawimbi machafu yaletayo dhoruba katika imani yetu.

Katika somo la kwanza tunaona Nabii Ayubu akituwekea mawazo ya watu wa kale juu ya bahari. Bahari ilieleweka kama ni kitu chenye ukorofi dhidi ya Mungu na hivi Mungu anaiwekea mipaka kwa sababu yeye ni mwenye nguvu. Anasema mawimbi yako ewe bahari yatakuwa na mwisho.

Somo hili la kwanza linaeleweka vema likiunganishwa na somo la Injili ambapo Bwana anakemea mawimbi ya bahari na bahari inatulia. Tendo hili la Mungu alilolitenda katika Agano la Kale na Jipya lataka kutufundisha nini? Latufundisha hali ya machafuko ya kiroho, kijamii, kijiografia na kiuchumi yaliyo masumbufu kwa jamii yetu. Haya ni mawimbi ya bahari, na hivi nani wa kuyakemea ni Mungu mwenyewe. Kumbe mwaliko ni kushika upendo kwa dhati na uhuru kamili wa wana wa Mungu. Ni kuwa na imani thabiti isiyo na shaka mpaka mwisho wa nyakati tukiamini lile fundisho la Bwana “nipo pamoja nanyi mpaka ukamilifu wa dahari” Mt. 28:16-20.

Katika Somo la Pili,  Mtume Paulo anapowaandikia Wakorinto anawahimiza kuweka katika maisha yao kumbukumbu ya imani yakuwa Kristu alikufa kwa ajili ya wote na hivi wao pia waishi upendo uliojaa ukarimu kwa ajili ya wengine. Kwa njia ya Kristu maisha mapya huanza na hukamilika, na hivi mwaliko ni kutoka maisha ya zamani na kuelekea maisha mapya tukiwa na matumaini katika Yesu Kristu mwokozi wa wote.

Katika Injili ambapo ndipo hasa kiini cha tafakari yetu tunawaona Mitume wakiwa na Bwana akiwa amesinzia katika mashua. Wakiwa wanaendelea na safari mara upepo mkali unatikisa mashua na Mitume wanaanza kuingiwa na woga. Tunajiuliza walikuwa wanaenda wapi? Wako katika utume wanaenda upande mwingine wa bahari kutangaza habari njema. Kumbe mashua ni Jumuiya ya Kikristu inayotangaza habari njema baada ya ufufuko wa Bwana. Hata hivyo jumuiya hii inakumbana na matatizo ndiyo dhoruba, ndiyo upepo mkali. 

Mwinjili anataka kutuambia matatizo kama vile, migawanyiko, majadiliano mbalimbali, uzushi na mengine kama hayo yaliyoikumba jumuiya ya kwanza ya kikristo. Bwana amelala ni alama ya kifo chake, hayuko tena nasi kama ilivyokuwa mwanzoni, lakini wanapomshitua anatenda kazi! Ni kwa namna gani twaweza nasi kumwita Bwana katika mawimbi makali? Ni kwa njia ya sala zetu za kila siku. Mashaka ya Mitume yashuhudia kuwa, peke yetu hatuwezi kitu lazima daima kumtegemea Mungu.

Mara kadhaa, tunaweza kuingia katika taabu ya kumwona Mungu ni wa maana wakati wa taabu tu, ni kweli, lakini yatupasa na inafaa kumwita Mungu kila dakika ya maisha yako kwa njia ya matendo yako na sala mbalimbali. Mungu si duka ambalo mtu huenda wakati analohitaji la kununua kitu fulani, bali Mungu ni kimbilio letu kila siku na kila saa kwa ajili ya kuokoa toka mawimbi dhidi ya mashua. Kumbe tukumbuke tukiwa na Mungu tuna nguvu na ushindi dhidi ya dhoruba na mitikiso mbalimbali katika maisha ya kuelekea mbinguni.

Ninakutakieni baraka tele za Mungu na imani thabiti daima ili maisha yako yaambatane na sala. Tumsifu Yesu Kristo. 

Tafakari imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.