2015-06-17 14:58:00

Siku ya Wakimbizi Duniani 2015: Bomoeni kuta zainazowatenga watu!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake kuhusu familia, Jumatano tarehe 17 Juni 2015 amekumbushia kwamba, Jumamosi iyajo, tarehe 20 Juni 2015, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wakimbizi na wahamiaji ambao wanajikuta wako mbali na nchi zao, wanafuta makazi ya salama bila ya kuwa na wasi wasi; ili waweze kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wao.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwatia shime wale wote wanaoendelea kuwasaidia wakimbizi kwa hali na mali. Anatumainia kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaweza kupata muafaka wa jinsi ya kuzuia watu kulazimika kuzikimbia nchi zao kwa nguvu.

Wakati huo huo, Chama cha Malta kimeanza kuendesha kampeni ya kimataifa kwa kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuonesha mshikamano wa upendo kwa wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta hifadhi ya maisha yao sehemu mbali mbali za dunia. Kamwe Jumuiya ya Kimataifa isijenge kuta za utengano bali mshikamano wa umoja, upendo na udugu. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna watu millioni 52 wanaolazimika kuyakimbizi makazi yao kutokana na majanga asilia.

Zaidi ya watu millioni 33 hawana makazi maalum. Takwimu zinaonesha pia kwamba, kuna watu millioni 1. 5 wanaomba hifadhi ya kisiasa, wengi wao ni wale wanaotoka Syria na Iraq, maeneo ambayo kwa sasa yanawaka moto wa vita na kinzani za kijamii. Chama cha Malta kwa miaka kumi, kimekuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha watu sehemu mbali mbali kuguswa na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi ya maisha ugenini. Kuna haja ya kuwa na mwelekeo mpya unaojikita katika huduma ya upendo na mshikamano.

Chama cha Malta kimekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji huko Uturuki na Syria; Sudan ya Kusini na Uganda; Nepal na Myanmar. Lengo ni kuhakikisha kwamba, utu na heshima ya wahamiaji na wakimbizi unazingatiwa pamoja na kupewa haki zao msingi. Wimbi kubwa la wahamiaji kutoka maeneo yenye vita na machafuko ya kisiasa ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kwa wakati huu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.