2015-06-17 15:28:00

Papa Francisko kuhiji Jimbo kuu la Torino: tarehe 21- 22 Juni 2015


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa jumapili ijayo tarehe 21 hadi tarehe 22 Juni 2015 kufanya hija ya kichungaji Jimbo kuu la Torino, Kaskazini mwa Italia, ili kwenda kutoa heshima yake kwenye Sanda Takatifu pamoja na kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 200 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Bosco, mtume wa vijana.

Atakapowasili mjini Torino, Baba Mtakatifu Francisko atapokelewa na viongozi wa Kanisa na Serikali ya Italia. Atazungumza na wafanyakazi na baadaye atakwenda kwenye Kanisa kuu la Torino, ili kusali na kutoa heshima yake kwenye Sanda Takatifu na baadaye atasali mbele ya kaburi la Mwenyeheri Giorgio Frassati, kielelezo makini cha majadiliano ya kina kati ya Kanisa  Katoliki na Ulimwengu kwa wakati ule. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, heshima kwa Sanda Takatifu itawasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuona sura ya Yesu Kristo inayoonesha upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani na kwa njia hii, wanaweza pia kuona sura ya ndugu zao wanaoteseka: kiroho na kimwili.  

Baba Mtakatifu kabla ya Ibada ya Misa Takatifu atasalimiana na Maaskofu watakaoshiriki katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, litakaloadhimishwa kwenye Uwanja wa Vittorio Veneto, Torino. Baba Mtakatifu baada ya misa, atasali na waamini Sala ya Malaika wa Bwana. Atapata chakula cha mchana na watoto waliofungwa kwenye Gereza la Watoto watukutu, la “Ferrante- Aporti”. Meza hii itapambwa pia na maskini na watu wasiokuwa na makazi, ambao wanaendelea kupewa kipaumbele cha kwanza na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, kwani anasema, maskini ni amana na hazina katika mchakato wa Uinjilishaji, pasi na maskini, ni vigumu sana kuifahamu Injili ya Kristo.

Baba Mtakatifu majira ya alasiri, atatembelea Madhabahu ya Bikira Maria wa Consolata na kusali huko katika faragha. Mapadre wanaohudumia madhabahuni hapo ndio wao peke yako walioruhusiwa kushiriki pamoja na Baba Mtakatifu. Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na Wasalesiani na Watawa wa Bikira Maria msaada wa Wakristo, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka mia mbili tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Bosco.

Baadaye atatembelea na kusalimiana na wagonjwa pamoja na walemavu watakaokuwa wamekusanyika kwenye Kanisa la Cottolengo. Hapa Baba Mtakatifu atasalimiana na kila mmoja wao, ili kuwatia shime kusonga mbele katika imani na matumaini. Baba Mtakatifu atakutana na kujibu maswali ya vijana kwenye Uwanja wa Vittorio.

Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Francisko atakavyokuwa anahitimisha siku yake ya kwanza Jimbo kuu la Torino. Usikose kujiunga na Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, itakapokuletea yale yatakayojiri, siku ya pili ya hija ya Baba Mtakatifu Francisko Jimbo kuu la Torino kama sehemu ya maadhimisho ya Miaka mia mbili tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Bosco pamoja na kutoa heshima yake kwa Sanda Takatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.