2015-06-17 14:42:00

Kifo na misiba inapotikisa familia, Yesu awe ni kimbilio la matumaini!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake, Jumatano, tarehe 17 Juni 2015 ameendelea kupembua kuhusu maisha na utume wa Familia, lakini kwa namna ya pekee, pale msiba na majonzi yanapongia na kuitikisa familia, kama inavyojionesha kwa Mama mjane wa Naini, ambaye mtoto wake wa pekee alifariki dunia na wakati wakiwa njiani kuelekea kwenye mazishi, wakakutana na Yesu aliyemwonea huruma, akagusa jeneza, akamponya yule kijana na kumrudisha kwa Mama yake, akiwa mzima.

Baba Mtakatifu anasema watu wote wakamtukuza Mungu, hali ambayo inaonesha nguvu ya Yesu dhidi ya kifo, ambacho kina wagusa wote pasi na ubaguzi. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, hakuna hata mtu mmoja anayeweza kujidai kwamba amezoea kifo, kwani kwa asili kifo hakizoeleki! Inasikitisha kuona familia ikimpoteza mtoto au moja ya wanafamilia wake. Maandiko Matakatifu anasema Papa Francisko yanashuhudia kwamba, Yesu daima anaendelea kufanya hija na waja wake, hata nyakati za giza kwa kuondokewa na wanafamilia, wakati wa majonzi na maombolezo.

Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na imani thabiti katika ufufuko wa wafu na uwepo wake endelevu wa Yesu Kristo na kwa njia hii, waamini wanaweza kupokea msiba kwa imani na matumaini kwani kamwe Yesu hawezi kuwaacha wale ambao amekabidhiwa na Baba yake wa mbinguni na hapo mwamini anaweza kuungana na Mtakatifu Paulo kwa kusema “Ku wapi, ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, ewe mauti, uchungu wako?

Waamini wanakumbushwa kwamba, mauti haina usemi wa mwisho katka maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kwa namna ya pekee, kuiga huruma na upendo wa Yesu, kwa kutambua namna ya kuwa karibu ili kuwafariji wale wanaoteseka kutokana na kuondokewa na ndugu na jamaa zao kutokana na kifo.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa upendo uliofunuliwa na Kristo kwa njia ya Fumbo la Msalaba, yaani mateso, kifo na ufufuko wake, kwa kutambua kwamba, upendo una nguvu zaidi kuliko kifo. Waamini waoneshe imani yao kwa Kristo, inayoweza kujibu matamanio yao ya ndani, wakati wanapokabiliwa na kifo cha ndugu na wapendwa wao. Anapenda kuwasindikiza kwa njia ya sala na sadaka yake, wale wote walioguswa na kutikiswa na misiba katika familia zao.

Viongozi wa Kanisa na Jumuiya za Kikristo katika ujumla wake ziwasindikize watu hawa kwa njia ya sala pamoja na kuwapatia msaada wa hali na mali, watambue kwamba, upendo wa huruma ya Mungu hauwezi kumtupa mtu kamwe. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko ameungana na waamini pamoja na mahujaji kutoka Poland wanaoadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Alberto Chmielowski, aliyejisadaka kwa ajili ya maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum; kwa kuwahudumia wagonjwa waliokuwa na magonjwa sugu, mwaliko kwa waamini kufungua malango ya mioyo yao kwa ajili ya kuwaonjesha maskini upendo na huruma ya Kristo 

Waamini wajifunze kumhudumia Kristo kwa njia ya maskini na hivyo watakuwa kweli ni “mkate” unaomegwa kwa ajili ya wengine. Wajitahidi kumuiga Kristo katika utakatifu wa maisha. Moyo Mtakatifu wa Yesu uwe ni chemchemi ya lishe ya maisha ya kiroho na matumaini kwa kuambata upendo wa Kristo.

Mwishoni, Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, Alhamisi asubuhi, atazindua rasmi Waraka wake wa kitume kuhusu utunzaji bora wa mazingira ambayo ni nyumba ya wote. Nyumba hii kwa sasa inaendelea kuharibika na athari zake zinawagusa na kuwatisa wote, lakini zaidi maskini.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, watu watawajibika kadiri ya dhamana na utume ambao Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu ailime na kuitunza bustani alimowekwa na Mungu. Anawahamasisha watu wote wenye mapenzi mema kuupokea Waraka huu kwa moyo mweupe kwani unakwenda sanjari na Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.