2015-06-17 08:38:00

Familia ni maabara ya utu na heshima ya binadamu; mahali pa malezi na makuzi


Maaskofu kutoka katika Makanisa ya Mashariki, hivi karibuni wamehitimisha mkutano wao, uliokuwa unafanyika mjini Prague, Jamhuri ya Watu wa Czech, kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, inayoongozwa na kauli mbiu wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo. Sinodi hii itaadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015.

Maaskofu pamoja na mambo mengine wamegusia kwa namna ya pekee: umuhimu wa kusimama kidete, kulinda, kutunza na kushuhudia tunu msingi za Injili ya familia inayojikita katika upendo wa dhati kati ya bwana na bibi. Wanazitaka Serikali kuwa na mwelekeo chanya zaidi kuhusiana na sera, sheria na mikakati ya ndoa na familia. Wameonesha mshikamano wao wa dhati na wananchi wa Ukraine wanaokabiliwa na maafa makubwa kutokana na vita. Maaskofu wanasema kwamba, Kanisa Katoliki katika baadhi ya nchi linabaguliwa na kutengwa, kwa vile linataka kusimamia mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu.

Maaskofu kutoka Ulaya ya Mashariki wanasema kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema hawana budi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwani familia ni maabara ya utu na heshima ya binadamu. Familia ni kiini cha maisha ya binadamu, mahali pa malezi na makuzi ya watoto; Kanisa la nyumbani na uwanja wa tunu msingi za maisha ya binadamu.

Familia ni mahali muafaka pa kurithisha imani, matumaini na mapendo, kwa kujifunza kupokeana, kuheshimiana na kuthaminiana; tayari kusaidiana kwa hali na mali. Familia zilizoungana na kushibana Barani Ulaya, zimekuwa kwa kiasi kikubwa kifungo cha upendo na mshikamano, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; uhuru na maendeleo ya wengi. Familia ni urithi mkubwa wa maisha ya binadamu: kiroho, kitamaduni na kiutu, kwa hakika familia inayoundwa kati ya bwana na bibi haina mbadala.

Hii ni changamoto kwa Familia za Kikristo kuhakikisha kwamba, zinaendelea kuwa hai na makini zaidi kwa kutetea, kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Jamii inataka kuona mifano hai, ili kuwapatia watu matumaini kwa siku za usoni.

Kama sehemu ya mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, Makanisa mahali yanaendelea kuhamasishwa, ili kuhakikisha kwamba, yanatoa kipaumbele cha kwanza katika utume wa familia. Maaskofu wakazie maandalizi ya kina kwa wanandoa watarajiwa ili waweze kutambua uzuri, ukuu na utakatifu wa maisha ya ndoa ya Kikristo.

Wanandoa watarajiwa wasindikizwe kikamilifu katika maisha yao ya kiroho, kiutu na kitamaduni, kwa kusaidiwa na vyama vya  utume Parokiani na Majimboni. Waamini waoneshe moyo wa upendo na mshikamano kwa familia zinazokabiliwa na mateso pamoja na mahangaiko mbali mbali; wawe tayari kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika ushuhuda wa maisha ya Kikristo.

Maaskofu wanakiri kwamba, nyakati hizi kuna wimbi kubwa la kumong’onyoka kwa maadili na utu wema; mambo yanayochangiwa kwa namna ya pekee na athari za myumbo wa uchumi kimataifa; kukengeuka kwa watu na kutopea katika dhambi kiasi cha kuathiri tunu msingi za maisha ya kijamii. Malezi na majiundo makini ni muhimu sana katika ustawi na maendeleo ya vijana wa kizazi kipya, ili kujenga na kudumisha mfungamano wa kijamii. Ukosefu wa fursa za ajira na tatizo la vijana kukimbia nchi zao ili kutafuta nafuu ya maisha ni changamoto kubwa katika maisha na utume wa Makanisa mahalia.

Maaskofu wanapenda kuonesha mshikamano wao wa dhati na Familia ya Mungu nchini Ukraine ambayo kwa sasa inateseka kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo ambayo imesababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Mateso na mahangaiko ya wananchi wa Ukraine si tena sehemu ya habari za kimataifa wanasema Maaskofu. Ili kweli amani, ustawi na maendeleo ya wengi yaweze kufikiwa, kuna haja kwa Familia ya Mungu nchini humo kujikita katika hija ya toba na wongofu wa ndani; kwa kuondokana na rushwa, ufisadi na tamaa ya mali na madaraka.

Maaskofu wanayataka Mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki yaendelee kutoa msaada kwa wananchi wa Ukraine hata wakati huu, watu wengi wanapoanza likizo ya kiangazi. Maaskofu wanasikitishwa sana na tabia ya baadhi ya viongozi wa Serikali kulibagua na kulitenga Kanisa katika masuala ya uchumi na fedha. Makanisa mahalia yanahamasishwa kujielekeza katika kanuni maadili, ukweli na uwazi kwa matumizi ya fedha za Serikali na umma, ili kweli haki iweze kutendeka.

Mkutano huu wa Maaskofu umehitimishwa kwa Ibada ya Neno la Mungu. Uliandaliwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, CCEE. Askofu mkuu Cyrl Vasil, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki ameshiriki na kutoa salam na ujumbe wa matashi mema kutoka kwa Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa Makanisa ya Mashariki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.