2015-06-16 08:48:00

Yesu Kristo aliyetundikwa Msalabani ni muhtasari wa wema na upendo wa Mungu!


Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani, changamoto na mwaliko kwa waamini kukimbilia huruma na upendo huu katika hija ya maisha yao. Ni maneno yaliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, mwishoni mwa juma, kama kielelezo cha kukamilisha hija ya kikazi huko kwenye Falme za Kiarabu, ambako pamoja na mambo mengine ameshiriki uzinduzi na hatimaye, kutabaruku Kanisa lililojengwa kwa heshima ya Mtume Paulo.

Ibada hii ya Misa takatifu imehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa kwenye Falme za Kiarabu pamoja na Familia ya Mungu nchini humo, ili kushiriki kikamilifu katika upendo wa Mungu kwa ajili ya wote. Huu ni upendo endelevu unaojikita katika uaminifu unaomkirimia mwamini  huruma, neema na utumilifu wa maisha. Kwa namna ya pekee, Yesu alijionesha si kwa mafundisho yake, wala kwa miujiza aliyowatendea watu, bali pale alipoinuliwa juu Msalabani, akainamisha kichwa na kukata roho, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu unaokoa na kuponya dhambi za mwanadamu.

Kardinali Parolin, katika mahubiri yake anasema kwamba, kwa mwamini anayetaka kufahamu, kuonja na kuukumbatia upendo na huruma ya Mungu, hana budi kumwangalia Yesu aliyetundikwa Msalabani, Yesu aliyetobolewa ubavu kwa mkuki, humo zikatoka Sakramenti za Kanisa. Waamini wajitahidi kumwomba Yesu katika sala na maisha ili awajalie kuwa na moyo mkuu unaoguswa na mahangaiko ya watu, hasa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kardinali Parolin, Jumamosi, tarehe 13 Juni 2015 amekwenda hadi Dubai na kuadhimkisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la Bikira Maria, kwa kufanya kumbu kumbu ya Moyo Safi wa Maria sanjari na kumbu kumbu ya Mtakatifu Antoni wa Padua. Anasema, Liturujia ya Neno la Mungu katika matukio haya mawili ilikuwa limesheheni roho na mafumbo yanayoonesha maisha na wito wa Bikira Maria; mwanamke mwenye imani kubwa, iliyomwezesha kuwa kweli ni Mama wa Mungu na Kanisa; akabarikiwa kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili.

Bikira Maria ni mfano na kielelezo cha maisha, wito na utume wa Kikristo. Ni Mama anayewaelekeza waamini kwa Yesu Kristo, Mkombozi wa dunia. Mtakatifu Antoni wa Padua ni maarufu sana sehemu mbali mbali za duni, wengi wanamtambua kuwa ni Padre mtakatifu, lakini kabla ya kuwa mtakatifu, alikuwa ni mwamini, aliyetambua dhamana na nafasi ya Roho Mtakatifu katika maisha ya kila mwamini na utume wa Kanisa.

Hii ni changamoto kwa Wakristo kuhakikisha kwamba, wanamwilisha imani yao katika matendo kwa njia ya ushuhuda makini, wenye mvuto na mashiko. Wawe ni watu wenye moyo wa Ibada kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ushuhuda na mifano bora ya maisha ya Kikristo. Kwa njia hii, waamini wanaweza kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu inayookoa na kuponya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.