2015-06-16 16:28:00

Rais Omar El Bashir wa Sudan achafua hali ya hewa kisiasa Afrika ya Kusini


Hali tete ya wakimbizi na wahamiaji kutoka Barani Afrika wanaoendelea kufa maji kwenye Bahari ya Mediterrania; machafuko ya kisiasa nchini Burundi yanayotishia amani na usalama wa Nchi zilizoko kwenye Ukanda wa Maziwa makuu; vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na Boko Haram na Al Shabaab Barani Afrika; ni kati ya mambo ambayo yametawala mkutano wa viongozi wakuu wa Nchi za Kiafrika katika mkutano wao wa siku mbili uliokua unafanyika mjini Johanesburg, Afrika ya Kusini.

Uwepo wa Rais Omar Hassam El Bashir wa Sudan umechafua hali ya hewa kwa Mahakama ya Uhalifu wa kivita, ICC kutaka akamatwe ili afikwishe mbele ya mkondo wa sheria kujibu kutuhuma za uhalifu wa kivita, jambo ambalo viongozi mbali mbali Barani Afrika hawaliungi mkono hata kidogo.

Tatizo na changamoto ya wahamiaji na wakimbizi limepewa kipaumbele cha pekee kwa Afrika ya Kusini kuwa ni kati ya nchi ambazo pia ziliguswa na kutikishwa kwa vitendo vya kikatili walivyofanyiwa wahamiaji na wakimbizi nchini humo. Kuna umati mkubwa wa wahamiaji unaoendelea kufa maji kwenye Bahari ya Mediterrania katika harakati za kwenda Ulaya.

Bara la Afrika halina budi kuibuka na mbinu mkakati utakaodhibiti wimbi la wahamiaji na wakimbizi, wanaoendelea kuteseka kwa kudhani kwamba, kuna maisha bora Ulaya na Marekani wanakokimbilia, lakini wanapofika huko wanajikuta wakikabiliwa na hali ngumu zaidi, kiasi hata cha utu na heshima yao kutiwa rehani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.