2015-06-16 09:02:00

Mwanadamu apewe kipaumbele cha kwanza katika mapambano dhidi ya baa la njaa!


Maendeleo endelevu hayapaswi kuwa ni sehemu ya mikakati ya kiuchumi peke yake, bali mchakato mzima unaopania kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na mgawanyo bora zaidi wa haki unaozingatia pamoja na mambo mengine sheria. Hiki ndicho kiini cha hotuba iliyotolewa na Monsinyo Fernando Chica Arellano, mkuu wa ujumbe wa Vatican kwenye mkutano mkuu wa thelathini na tisa wa Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO uliohitimishwa hapo tarehe 13 Juni 2015 hapa mjini Roma.

Monsinyo Arellano ambaye ni mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO, anasema kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuhakikisha kuwa inaivalia njuga changamoto ya maendeleo endelevu ya kilimo pamoja na baa la njaa kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mahitaji ya binadamu, utu na heshima yake. Hii ni dhamana nyeti na endelevu kwa nchi husika na kwa Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake.

Monsinyo Arellano anasema, FAO licha ya kuangalia takwimu za mafanikio yaliyokwishafikiwa hadi sasa, ina haja ya kuwa na mwelekeo mpana zaidi ili kuibua mbinu mkakati utakaoiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kupambana kikamilifu na changamoto zinazoendelea kuibuliwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Hapa mkazo ni kutaka kutoa kipaumbele cha pekee kwa ugavi wa haki unaoambata misingi ya FAO.

Kutokana na changamoto hii, mikakati ya maendeleo haina budi kuangaliwa kama sehemu ya mchakato wa maendeleo ya ulimwengu mzima, yanayoweza kufikiwa kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi. Ikiwa sera na mikakati ya maendeleo itashindwa kuwa na mwelekeo huu, madhara yake ni makubwa katika ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.