2015-06-16 15:22:00

Gusweni na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi!


Askofu mkuu Jean Claude Hollerich wa Jimbo kuu la Lusenburg ambaye pia ni Rais wa Shirika la haki na amani Barani Ulaya,” Iustitia et pax Europa” hivi karibuni katika mahubiri yake kama sehemu ya maadhimisho ya miaka thelathini tangu Nchi za Ulaya ziliporidhia Mkataba wa Schengen, hapo tarehe 14 Juni 1985, amezitaka nchi wanachama kuhakikisha kwamba, zinaendelea kukumbatia na kuenzi ule moyo wa upendo na mshikamano ulioneshwa na waasisi wa mktaba huu kwa kutoa uhuru wa watu kuweza kusafiri Barani Ulaya pasi na kikwazo.

Askofu mkuu Jean Claude Hollerich anasema, uhuru wa mtu kutembea bila vikwazo, unapaswa pia kutolewa si tu kwa wananchi wa Bara la Ulaya, bali hata wale waliobahatika kufika Ulaya; wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi ya maisha yao kutokana na vita, nyanyaso, madhulumu na majanga mbali mbali ya maisha. Nchi wanachama wa Schengen wamefanya kumbu kumbu ya uhuru wa kutembea Barani Ulaya wakati ambapo kuna makundi makubwa ya wahamiaji ambayo yamenyimwa nafasi ya kuvuka na kuingia katika baadhi ya nchi za Ulaya.

Viongozi wa Jumuiya ya Ulaya wanaendelea kukuna vichwa ili kuangalia ni kwa jinsi gani wanaweza kufikia muafaka katika sera na mikakati ya kuwahudumia wahamiaji na wakimbizi wanaoendelea kuingia kwa wingi Barani Ulaya kutoka katika nchi ambazo kwa sasa kuna vita na machafuko ya kijamii. Viongozi wa Kanisa wanaitaka Jumuiya ya Ulaya kuonesha mshikamano kwa kujali na kuguswa na mahangaiko ya watu wanaotafuta hifadhi ya maisha yao  kwa kukimbia kutoka katika maeneo ya vita na kinzani za kijamii.

Askofu mkuu Jean Claude Hollerich anakaza kusema, Bara la Ulaya haliwezi kuwa mtetezi wa haki, amani na mshikamano kati ya watu ikiwa kama ubinafsi wa kitaifa unatawala kati ya nchi wanachama, kiasi cha kushindwa kuona wala kuguswa na mahagaiko ya wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Wakuu wa nchi zinazounda mkataba wa Schengeni wanapaswa kuzingatia na kusimamia ukweli juu ya uhuru wa watu kutembea Barani Ulaya; kwa kutenga walau asilimia 0.7% ya Pato Ghafi la Taifa kwa ajili ya kusaidia mchakato wa maendeleo ifikapo mwaka 2020.

Hakutakuwepo na amani  wala utulivu, ikiwa kama mamillioni ya watu yataendelea kutumbukizwa katika baa la umaskini wa hali na kipato; njaa na utapiamlo wa kutisha. Wahamiaji na wakimbizi wataendelea kuongezeka maradufu, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inajenga utandawazi wa mshikamano kwa kuguswa na mahangaiko ya maskini  na wote wanaoendelea kugalagazwa kutokana na umaskini na baa la njaa duniani.

Sera na mikakati ya maendeleo itoe kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na ustawi wa mwanadamu: kiroho na kimwili. Hivi ndivyo Askofu mkuu Jean Claude Hollerich anavyohitimisha mahubiri yake, wakati huu Jumuiya ya Ulaya inapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka thelathini tangu baadhi ya nchi za Ulaya zilizotia mkwaju, Mkataba wa Schengen unaowapa ruhusa wananchi Barani Ulaya kutembea kwa uhuru pasi na kizuizi chochote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.