2015-06-15 14:25:00

Wazazi wanaopendana na kushibana ni mashuhuda wazuri wa Injili ya Familia


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni tarehe 14 Juni 2015 amefungua rasmi kongamano la Jimbo kuu la Roma kwa kukutana na umati wa familia kutoka Jimbo kuu la Roma, waliokusanyika kusali kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kongamano hili linaendelea kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano na baadaye wajumbe wataweza kutoa mwelekeo wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa Mwaka 2015 – 2016; mikakati itakayojadiliwa kwa kina tarehe 14 Septemba 2015 kwa kuwashirikisha Wakleri na baadaye waamini walei.

Kongamano hili linaongozwa na kauli mbiu “tunawatangazia kile ambacho tumerithi. Sisi wazazi ni mashuhuda wa uzuri wa maisha”. Kwa hakika wazazi na watoto wamekuwa ni wahusika wakuu katika mkutano huu ambao Baba Mtakatifu amewataka wazazi kujibidisha zaidi katika kutoa malezi kwa watoto wao, wanaporejea kutoka shuleni, kama sehemu ya mchakato wa kupyaisha maisha ya kimaadili na kiroho kwa Jiji la Roma. Maadhimisho ya Sinodi ya familia yanalenga kuwasaidia waamini kutambua uzuri na wito wa maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu, ili waweze kuwa kweli waaminifu na wadumifu kadiri ya mpango wa Mungu.

Upendo huu uwe ni kiini cha sadaka na majitoleo ya wazazi kwa watoto wao ndani ya familia; wawe ni mfano na kielelezo hai cha ubaba na umama katika familia, kielelezo cha Injili ya familia inayotangazwa na kushuhudiwa kwa njia ya maisha adili na matakatifu. Maisha ya ndoa na familia ni wito mtakatifu kutoka kwa Mwenyezi Mungu unaopania pamoja na mambo mengine, kurithisha zawadi ya maisha, kwa kushiriki katika kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amepewa dhamana hii nyeti na Mwenyezi Mungu. Kwa wito wa kuwa Baba na Mama wa Familia, wanafananishwa na Mwenyezi Mungu, Muumbaji.

Familia anasema Baba Mtakatifu, zinapaswa kuwa ni chemchemi ya haki, amani na upendo na wala si uwanja wa masumbwi na mafarakano, mambo ambayo yanaacha Kurasa chungu katika maisha ya watoto. Watoto wanataka kuwa na mazingira ya amani, utulivu, upendo na furaha inayobubujika kutoka kwa wazazi wao. Lakini kwa bahati mbaya, watoto wamekuwa ni waathirika wa kinzani na migogoro ya kifamilia sehemu mbali mbali za dunia. Wazazi wajenge utamaduni wa kupendana na kuheshimiana; kusameheana na kusaidiana katika maisha, kwa njia hii hata watoto wao wataweza kujifunza tunu msingi za maisha.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha kwamba, wazazi wanao wajibu wa kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano kama kielelezo cha Fumbo la Utatu Mtakatifu. Huu ndio msingi unaoweza kutumika kujenga wito wa maisha ya ndoa na familia. Huu ni upendo shirikishi kati ya wanandoa, kwa kukamilishana na kusaidiana wakati wa raha na shida, wote kwa pamoja wakipania kuelekea katika utakatifu wa maisha. Wanandoa katika utofauti wao, wanakamilishana na kutegemezana; ili kuwa tayari kusamehe na kuanza upya pale wanapofarakana kama binadamu, ili kuendelea kumwilisha upendo unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ndoa Takatifu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, hata wale wanandoa ambao wametengana, bado Kanisa linawabeba na kuwakumbatia moyoni wake, linataka kuwasaidia na kuwashirikisha maisha na utume wa Kanisa. Hii ni changamoto kubwa katika maisha ya ndoa na familia kwani madhara yake ni mateso na mahangaiko ya watoto. Huu ni mwaliko wa kukumbatia mchakato wa msamaha na upatanisho, kwa kutambua mapungufu ya binadamu, tayari kuombana toba na msamaha wa kweli. Watoto wakionjeshwa upendo, wanaweza kuwa kweli ni chachu ya umoja na mshikamano ndani ya familia.

Baba Mtakatifu anawapongeza mababu na mabibi wanaoendelea kuchangia kwa hali na mali ustawi na maendeleo ya familia za ndugu na jamaa, changamoto ya kuhakikisha kwamba, wanathaminiwa na kupendwa, kwani hawa ni maktaba muhimu sana katika kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni kwa vijana wa kizazi kipya. Hata katika uzee wao wapendwe na kuthaminiwa na kamwe wasionekane kuwa kama mzigo na watu wa kubwezwa kana kwamba si mali kitu ndani ya jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.