2015-06-15 15:13:00

Wakristo shikamaneni ili kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo!


Wananchi wa Jamhuri ya watu wa Czec wanaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 600 tangu alipofariki dunia Jan Hus, wana mapinduzi, kwa kufanya hija ya maisha ya kiroho na liturujia ya upatanisho mjini Roma, changamoto na mwaliko wa kujenga na kuimaarisha mahusiano kati ya Jumuiya mbali mbali, daima wakijitahidi kutii mapenzi ya Yesu, aliyewataka wafuasi wake kuwa wamoja.

Wakristo hawana budi kutambua kwamba, wanahamasishwa na Mama Kanisa kujenga na kuimarisha ushirikiano kati yao, kwa kuyaangalia matukio yaliyopita kwa mwanga mpya, ili hatimaye, kufikia muafaka, utakaowawezesha waamini kuungama kwa pamoja Imani katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ambalo kwalo, wamebatizwa na kupata maisha mapya; ubatizo kiwe ni kiungo cha udugu katika Kristo.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa wajumbe kutoka Jamhuri ya Watu wa Czec wakati wa hija ya upatanisho mjini Roma. Imekwishagota miaka mia sita, tangu alipofariki dunia Jan Hus, Mhubiri na mkuu wa Chuo kikuu cha Prague, Jamhuri ya Watu wa Czec. Kunako mwaka 1999, Mtakatifu Yohane Paulo II katika hotuba yake, alilaani kwa nguvu zote mauaji ya kikatili yaliyofanywa dhidi ya Jan Hus, mmoja kati ya waasisi wa mageuzi makubwa ndani ya Kanisa.

Kwa miaka mingi anasema Baba Mtakatifu Francisko, Jan Hus amekuwa ni kikwazo cha mahusiano mema kati ya Wakristo, lakini leo hii, ni chachu ya majadiliano, jambo muhimu sana katika huduma ya Kanisa linalotaka kujikita katika ukweli wa kihistoria kwa ajili ya Wakristo wote ndani na nje ya mipaka ya Jamhuri ya Watu wa Czec.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Waraka wao juu ya majadiliano ya kiekumene wanasema kwamba, uaminifu kwa wito wa Kanisa ni kiini cha majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa. Leo hii anasema Baba Mtakatifu Francisko, kuna haja kwa Wakristo kushikamana kwa dhati katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, ili kuweza kuwatangazia Watu  wa Mataifa, Injili ya Furaha, dhamana inayohitaji umoja na mshikamano miongoni mwa Wakristo, ili watu waweze kuamini katika mchakato wa Utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu.

Wakristo wanahamasishwa kuendelea kujikita katika wito wao kwa kuambata toba na wongofu wa ndani, ili kwa pamoja waweze kufanya hija ya upatanisho na amani. Katika safari hii ndefu anasema Baba Mtakatifu, Wakristo kwa njia ya neema ya Mungu wajifunze kuwa marafiki na kutoa nafasi kwa wengine, ili kujenga mahusiano ya dhati kuanzia katika ngazi za Jumuiya mahalia na Parokia. Liturujia ya Upatanisho wanayoiadhmisha mjini Roma, iwasaidie kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa kutambua kwamba, wote ni wadhambi, wanahitaji pia kuwasamehe wale waliowakosea.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.