2015-06-15 14:56:00

Mwanadamu apewe kipaumbele cha kwanza na wala si mafuta na biashara ya silaha


Shirika la Misaada kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, ROACO, Jumatatu tarehe 15 Juni 2015 limeanza mkutano wake wa themanini na nane, uliofunguliwa kwa hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko aliyekazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa kuendeza mchakato wa upatanisho, haki na amani huko Mashariki ya kati, eneo ambalo limekumbwa na majanga ambayo kwa sasa yanaonekana kana kwamba, hayawezi kupata ufumbuzi wa kudumu.

Mashariki ya Kati ni eneo ambalo limesheheni wakimbizi na wahamiaji na linaendelea kulowanishwa kwa damu ya mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. ROACO ni shirika ambalo linaendelea kutekeleza dhamana na utume wake katika ukimya kwa kusikiliza na kujibu kilio cha mahangaiko ya watu kwenye Makanisa ya Mashariki. Wananchi wa Iraq na Syria wanahitaji msaada, lakini zaidi wana kiu ya kuona: haki, amani na utulivu vikitawala tena katika nchi zao.

ROACO inatekeleza dhamana hii kwa niaba ya Kanisa ambalo linapenda kuangalia kwa jicho la ukweli, mateso na mahangaiko ya mwanadamu, madonda ya watu wanaonyimwa haki zao msingi pamoja na kunyanyaswa utu wao; Kanisa linapenda kusikiliza kilio cha watu hawa na kuwapatia jibu makini, ili kukuza umoja, urafiki na udugu, tayari kujikita katika mchakato unaopania kuvunjilia mbali kuta za utengano, ambao mara nyingi unafumbata unafiki na ubinafsi.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, inaoneka kuwa, Jumuiya ya Kimataifa katika siku za hivi karibuni imefungua macho yake, kwa kuona na kushuhudia uwepo wa Wakristo kwa miaka mingi huko Mashariki ya Kati. Jitihada zinaendelea kufanyika ili kutoa msaada kwa watu wanaodhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Hapa kuna haja ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia badala ya kugubikwa na uchu wa kutafuta mafao binafsi yanayotokana na nishati ya mafuta pamoja na biashara haramu ya silaha ambayo inaendelea kunuka damu ya watu wasiokuwa na hatia huko Mashariki ya Kati. Watu wanatangaza haki na amani, lakini kwa upande mwingine wanaendelea kukuza biashara  haramu ya silaha.

Pamoja na kuendelea kutoa huduma ya msaada wa Kikristo, lakini bado kuna haja ya kushutumu mambo yote yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu anasema, kuna haja pia ya kuendelea kuangalia maisha na utume wa Kanisa huko Ethiopia. Eritrea na Armenia; Makanisa makuu yanayojitegemea kisheria, lakini bado yanafungamanishwa na Mapokeo ya Kialexandria.

Ni wajibu wa ROACO kuzisaidia Jumuiya hizi za Kikristo kutambua kwamba, zinashiriki kikamilifu katika utume wa Uinjilishaji, kwa kuwapatia vijana wa kizazi kipya matumani na mwelekeo wa ukuaji, ili kukabiliana na changamoto ya vijana kukimbia nchi zao ili kutafuta maisha bora zaidi,  kwa kuhatarisha maisha yao kwenye Bahari ya Mediterannia.

Armenia ni nchi ambayo ilibahatika kupokea Ubatizo kwa miaka mingi na ina utajiri mkubwa wa historia, tamaduni na imani na ushuhuda. Msaada wa Kanisa katika eneo hili unapania kujenga na kudumisha umoja unaonekana miongoni mwa Wakristo, ili vijana wa kizazi kipya kutoka Armenia waweze kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi na kwamba, sadaka ya Wakristo wengi iwe ni mbegu ya haki na amani. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano wa themanini na nane wa ROACO kwa sala ya Mtakatifu Efrem, anayewaombea watu wake wokovu na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.  








All the contents on this site are copyrighted ©.