2015-06-15 14:45:00

Msiwe watu wa kupenda kulipiza kisasi! Bali wanyenyekevu na wapole!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 15 Juni 2015 amewataka waamini kulinda na kutunza mioyo yao dhidi ya mambo ya kidunia kwa kuambata neema na baraka zinazobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Hii ni changamoto ambayo inabubujika kutoka katika Liturujia ya Neno la Mungu, kwa mwaliko kutoka kwa Mtakatifu Paulo kwa waamini kukumbatia zawadi na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuonesha moyo wazi usiokuwa na maa!

Kila wakati, Mwenyezi Mungu anawajaliwa watu wake neema na baraka, ambazo hazipaswi kuwa ni kikwazo wala kizingiti kwa jirani, kwa kutomwilisha zawadi na neema hizi katika uhalisia wa maisha yanayojikita katika utakatifu. Maneno na matendo ya Wakristo yaoneshe na kushuhudia neema iliyoko ndani mwao na kwa jinsi hii wanaweza kuwa ni msaada mkubwa kwa jirani zao, jambo la msingi ni kutambua zile nyakati ambazo Mwenyezi Mungu anapita katika mioyo yao.

Waamini wawe makini kuhakikisha kwamba, analinda na kuutunza moyo wake, tayari kusikiliza kwa makini na kutunza amani ya ndani inayowaondolea vishawishi vya kutaka kulipiza kisasi, kama inavyooneshwa kwenye Maandiko Matakatifu, jicho kwa jicho, jino kwa jino! Badala yake, wawe ni watu wenye huruma, upendo na msamaha, tayari kuonesha shavu la pili, kielelezo cha unyenyekevu na upole.

Moyo wa mwamini hauna budi kulindwa dhidi ya vishawishi vinavyosababisha vita, kinzani na mapambano yasiyokuwa na mashiko. Hizi ni kelele za kipagani na kishawishi cha Shetani mwovu. Wakristo wawe tayari kushuhudia Ukristo wao kwa maisha matakatifu na adili, ili kutoa nafasi kwa uwepo wa Mungu katika maisha yao wakati wa shida na mahangaiko; wakati wa mateso, kukesha na kufunga. Wawe tayari kudumisha hekima, moyo mkuu, wema na utakatifu wa maisha. Unyenyekevu, uvumilivu na moyo mkuu ni mambo ambayo Mwenyezi Mungu anayaangalia anapopita katika moyo wa mwamini anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.