2015-06-15 16:39:00

Mchakato wa upatanisho na amani ya kudumu, mambo muhimu yaliyojadiliwa Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu asubuhi amekutana na kuzungumza na Rais Juan Manuel Santos Calderon wa Jamhuri ya Watu wa Colombia, ambaye baadaye amekutana pia na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Viongozi hawa katika mazungumzo yao, wameridhishwa na uhusiano mwema uliopo kati ya pande hizi mbili pamoja na kuonesha msisitizo wa mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Colombia katika ujumla wao; mchango unaojikita katika masuala ya kijamii na kitamaduni. Kwa namna ya pekee viongozi hawa wamejadili kwa kina mapana mchakato wa upatanisho wa kitaifa unaoendelea nchini Colombia, matatizo na changamoto zilizopo, ili kuweza kufikia mkataba wa amani ya kudumu.

Baba Mtakatifu Francisko pamoja na mgeni wake, wamebadilishana pia mawazo kuhusiana na hali ya kimataifa na kikanda hususan katika masuala ya kisiasa na kijamii, kwa kujikita zaidi katika hamu ya kuimarisha amani na utulivu katika eneo hili, sanjari na utekelezaji wa sera na mikakati ya maendeleo inayopania kudumisha usawa na ujenzi wa utamaduni wa utawala wa sheria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.