2015-06-15 09:16:00

Mchakato wa ujenzi wa jamii inayojikita katika maridhiano, haki, umoja na udugu


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, hivi karibuni ameshiriki katika uzinduzi wa Kanisa lililojengwa kwa heshima ya Mtume Paulo huko Abu Dhabi, Falme za Kiarabu, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa jamii inayojikita katika misingi ya maridhiano, haki, umoja na mshikamano wa kidugu, licha ya tofauti msingi zinazoweza kujitokeza.

Uzinduzi wa Kanisa hili ambalo limejengwa kwenye eneo la viwanda huko Mussafah, Abu Dhabi umehudhuriwa na viongozi wakuu wa Falme za Kiarabu. Siku iliyofuata yaani, Sherehe za Moyo Mtakatifu wa Yesu, Kardinali Parolin, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la Mtakatifu Paolo mjini Abu Dhabi na kulitabaruku tayari kwa ajili ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa.

Katika mahubiri yake kwenye Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kisima cha neema, huruma na upendo wa Kristo kwa waja wake, Kardinali Parolin, amewashukuru na kuwapongeza viongozi wa Kanisa walioshughulikia mradi huu hadi umekamilika. Wakristo wanahamasishwa kuendelea kushiriki katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa kwa kutambua kwamba, Yesu Kristo ndiye lile jiwe kuu la msingi.

Kardinali Parolin anasema kwa masikitiko kwamba, binadamu ni kutokana na ubinafsi na dhambi, ni mwepesi sana kuvunja na kuvura mambo. Lakini pamoja na kinzani, vurugu na nyanyaso mbali mbali, Yesu Kristo bado anaendelea kuwavuta wote kwake, ili kuonja huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka. Waamini watambue kwamba, mioyo yao ni Hekalu la Fumbo la Utatu Mtakatifu na kwamba, Yesu Kristo anaendelea kufanya hija pamoja na waja wake katika maisha yao ya kila siku. Kumbe, utofauti unaojionesha katika lugha, jamaa na taifa uwe ni chachu ya hekima, utakatifu na neema, ili kwa pamoja waweze kujisikia kuwa kweli ni Watoto wa Mungu, wafuasi na marafiki wa Yesu Kristo.

Itakumbukwa kwamba, tukio hili la kihistoria linafanyika baada ya kuyoyoma miaka 50 tangu Kanisa la kwanza lilipojengwa na kuwekwa wakfu kwenye Falme za Kiarabu kwa ajili ya maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa. Hili lilikuwa ni Kanisa la Mtakatifu Yosefu lililojengwa kunako mwaka 1965. Sasa Wakristo wanaweza kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa kuwa na Makanisa mawili, kwani idadi yao inaendelea kuongeza mwaka hadi mwaka kutokana na wahamiaji na wageni wanaotafuta fursa za ajira kwenye Falme za Kiarabu.

Kardinali Parolin amewashukuru viongozi wa Falme za Kiarabu kwa kuonesha utayari wa kushirikiana katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi; kwa kukuza na kuimarisha uhuru wa kidini; haki na amani; maridhiano na udugu kati ya watu wa mataifa, ili waweze kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Kardinali Parolin amemwimbia Mwenyezi Mungu wimbo wa sifa na shukrani kwa kuwakutanisha watu kutoka katika makabila, lugha na jamaa, ili kushiriki katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, wakiwa wameungana pamoja kama Familia inayojikita katika imani. Ni matumaini ya Kardinali Parolin kwamba, wakristo hao wataendelea kukua na kukomaa katika imani, matumaini na mapendo, tayari kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.